NI KUFUATIA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA NA KUSABABISHA ATHARI KUBWA IKIWEMO WATU WAWILI KUPOTEZA MAISHA.
Watu wawili Wilaya ya Kinondoni wanasadikiwa kupoteza maisha kufuatia mvua kubwa zinazoendele kunyesha katika jiji la Dar es salaam
Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Alli Hapi alipofanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo kwa lengo la kujionea hali halisi ya athari zilizosababishwa na mvua.
"Leo kama mnavyofahamu kumekuwepo na mvua ambazo zimeleta madhara makubwa katika Wilaya yetu ya Kinondoni, ziko taarifa ambazo zimethibitisha mpaka sasa tunao wananchi wawili ambao wamepoteza maisha kutokana na mvua ambazo zinaendelea, tunaendelea kukusanya taarifa kutoka maeneo mengine kupitia jeshi la polisi lakini mpaka sasa idadi iliyothibitika ni wawili," Amebainisha Hapi
Amesema takribani nyumba mia moja zimebomoka kufuatia mvua hizo na nyingine mia saba kuzungukwa na maji kitu ambacho kimeleta athari kwa wananchi waliowengi katika maeneo hayo.
"Tunazo nyumba ambazo ni zaidi ya mia saba ambazo zinakadiriwa zimezungukwa na maji lakini kadhalika tunazo nyumba zaidi ya mia moja ambazo zinasadikika zimebomoka katika kata zetu zote na katika mitaa mbalimbali ya Wilaya ya Kinondoni, mvua ambazo zimenyesha zimeleta madhara makubwa sana "Amesema Hapi .
Aidha amewataka Maafisa Mipangomiji wa Manispaa kuhakikisha wanafuatilia uhalali wa maeneo hayo kwa ramani za Mipangomiji na kujiridhisha kama maeneo hayo yaliyoathirika yalitengwa kwa ajili ya makazi ya watu.
"Maafisa Mipangomiji, angalieni uhalali wa maeneo haya, yalitengwa kwa matumizi gani "Alisisitiza Hapi
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa sheria, Mwananchi yeyote anapaswa kujenga umbali wa mita 60 kutoka chanzo cha mto.
Katika hatua nyingine amewataka wananchi waliojenga maeneo hatarishi kuhakikisha wanachukua tahadhari ili kuepukana na madhara yanayoweza kutokea kufutia mvua hizi zinazoendelea kunyesha.
"Wako baadhi ya wananchi wetu ambao wamejenga katika meneo yasiyoruhusiwa kisheria, kule mbezi kunawanchi wamejenga kandokando ya mto na sheria yetu inasema mita 60 kutoka chanzo cha mto haparuhusiwi kujengwa nyumba yeyote, wako baadhi ya wananchi wamejenga kwenye mabonde, maeneo ya mkondo wa maji maeneo ya mabonde na mabwawa hawa ndio wananchi ambao wamekuwa wahanga wakubwa sana wa mvua hizi ambazo zinaendelea kwa hiyo nitoe wito tu kwa wanachi wote ambao wako katika meneo hatarishi, waondoke haraka kupisha yanayoweza kujitokeza, wenzetu wa hali ya hewa wanasema mvua hizi zinaweza kuendelea na zinaweza kushika kasi zaidi ya hapa tuliposhuhudia"Amesisitiza Hapi.
Ametoa wito kwa wananchi kuvuta subira wakati Serikali inajipanga kutatua changamoto zilizotokana na mvua hizo na mamlaka husika kupiga dawa kwenye mabwawa, na madimbwi ikiwa ni pamoja na kusafisha mitaro kama hatua za awali za kujilinda dhidi ya mgonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Maeneo aliyoyatembelea Mkuu huyo wa wilaya ni Boko basihaya lililopo kata ya Bunju, Mto Nyakasangwe, Mto Mpiji ulioko Kata ya Mbweni, Daraja la Mbezi, eneo la Msisiri b, lililoko Kata ya Mwananyamala.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.