Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Ali Hapi leo amefanya ziara kukagua hatua mbalimbali za utekelezaji zilizofikiwa katika ukarabati wa barabara unaoendelea kwenye Wilaya yake ikiwamo zile zilizoko chini ya TARURA pamoja na zile zinazotekelezwa chini ya mradi wa DMDP.
Akikagua barabara hizo Mh Hapi amesema amefurahishwa na hatua zilizofikiwa na zenye viwango vya kuridhisha kwani kukamilika kwake kutawaondolea kero watumiaji wake hasa ile wanayoipata wakati wa mvua.
"Nataka niwaambie wananchi wa Kinondoni kuwa mwaka 2018, ni mwaka wa barabara, nimefanya ziara hii kujionea mwenyewe hatua za utekelezaji wa ukarabati, nimeridhishwa nao, niwaombe TARURA waharakishe upitiaji wa mikataba ya awali iliyoingiwa kuhusiana na barabara hizi na wanipatie majibu ndani ya kipindi kifupi
Naye Maneja TARURA Manispaa ya Kinondoni Mhandisi Leopod Rungi amebainisha kuwa takribani shilingi bilioni 1.2 zimetengwa kwa ajili ya kukarabati mita 22,000 za ukubwa ambapo ni sawa na urefu wa km 2.5 za barabara.
Ameainisha kazi zinazofanyika katika barabara hizo kuwa ni kuziba viraka, kufukia mashimo, usanifu pamoja na kutengeneza mitaro.
Katika hatua nyingine Mh Hapi amewataka wananchi kuhakikisha wanazithamini na kuzipenda barabara hizo kwa kuhakikisha wanazingatia usafi hasa yale maeneo ya mitaro yanayopakana na nyumba zao.
Barabara zilizotembelewa ni Barabara ya kondoa yenye urefu wa km 1.5, barabara ya mlandizi yenye urefu wa km 5.2, Barabara ya Sayansi yenye urefu wa km 0.6, barabara ya Slip way yenye urefu wa km 2.4, pamoja na barabara ya CCBRT yenye urefu wa km 0.8.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.