Maeneo hayo yametangazwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Godwin Gondwe alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ya ukaguzi wa miradi ya upanuzi wa barabara inayosimamiwa na Tanroads kwa lengo la kujiridhisha na hatua za utekelezaji zilizofikiwa, ikiwa ni pamoja na thamani ya fedha na kiwango cha mradi katika ubora.
Amesema kutangaza kwa maeneo haya ya Magomeni mataa hadi Morroco na Morroco hadi Mwenge kuwa maeneo maalumu "smart area" ni katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Kassim la kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na eneo kwa ajili ya vivutio vya utalii.
Aidha ameongeza kuwa maeneo haya yanatakiwa kutunzwa kwa kufanyiwa Usafi, kupendezeshwa kwa kuotesha maua na nyasi, kutokubadilishwa mandhari yake ikiwa ni pamoja na kutokuwepo uharibifu wowote pembezoni mwa barabara.
" Tanroads hakikisheni mnasimamia suala la wamachinga kwenda eneo walilopangiwa ili kupisha ujenzi na ukamilishaji wa barabara unaoendelea kwa sasa, lakini pia simamieni Mradi huu wa barabara unaopita eneo la Morroco hadi Mwenge ukamilike kwa wakati, barabara hii itunzwe na iheshimike ili wananchi wanufaike, tusingependa eneo hili liharibiwe, lichafuliwe, bali liboreshwe na kutunzwa, nalitangaza Rasmi kuwa "smart area" Ameongeza Gondwe.
Naye Mhandisi kutoka Tanroads Bi. Mwanaisha Rajab alipotakiwa kuzungumza amesema anayapokea maelekezo yote kutoka kwa uongozi na kuhakikisha miradi yote ya barabara inayosimamiwa na Tanroads kwa Manispaa ya Kinondoni inamalizika kwa wakati kutokana na makubaliano ya mkataba na kwa viwango vilivyokusudiwa ili viweze kuleta tija kwa maslahi mapana ya wananchi wa Kinondoni na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya Mhe. Godwin Gondwe amezitaka Taasisi na mamlaka husika zikiwemo Tanesco na Dawasco kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha miradi ya Serikali inatekelezwa ili iweze kuondokana na changamoto zinazoweza kukwamisha utekelezaji wake kwa viwango vilivyokusudiwa na yenye kuleta tija kwa Taifa.
Katika ziara hiyo iliyohusisha Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya imetembelea mradi wa upanuzi wa barabara ya Morroco-Mwenge yenye urefu wa Km 4.3, barabara ya Ardhi-Makongo yenye urefu wa Km 4.5, na barabara ya Madale.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.