Manispaa ya Kinondoni imesaini mkataba wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata taka kitakachojengwa eneo la Mabwepande na kitagharimu shilingi takriban Bilioni 5.56 hadi kukamilika kwake.
Mkataba huo umesainiwa leo na Mstahiki Meya Manispaa ya Kinondoni Mh. Benjamin Sitta na kushuhudiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo pamoja na wajumbe wengine katika tafrija iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
Akisaini mkataba huo amesema kiwanda hiki kinatarajiwa kumalizika ndani ya miezi kumi na nane kuanzia tarehe ya mkataba huu na kinatarajiwa kutengeneza tani hamsini mpaka mia moja za mbolea ya mboji kwa siku.
Ameongeza kuwa kiwanda hiki kitakuwa kinazalisha mbolea ya mboji itakayotumika kuongeza ukuaji mzuri wa mimea na kurudisha rutuba kwenye udongo uliokosa virutubishi na kuharibika.
"Mboji ni njia rahisi ya kuongeza rutuba kwenye udongo, na kusababisha ukuaji mzuri wa mimea, kuongezeka kwa mazao na kurudisha rutuba kwenye udongo ulioharibika na kukosa virutubishi "Amesisitiza Meya
Amezitaja faida zitakazopatikana na mboji hiyo itakayotengenezwa na kiwanda hicho cha kuchakata taka kuwa ni kusaidia mimea kukua vizuri wakati wa ukame, kusaidia mzunguko wa hewa kwenye udongo, kupunguza uchafu unaotupwa kwenye madampo pamoja na kuzuia uchafu wa Mazingira.
Katika hatua nyingine Meya Sitta ameainisha faida zitakazopatikana kutokana na kiwanda hicho kuwa kwanza ni sehemu ya mchango mkubwa katika Maendeleo ya nchi yetu katika kipindi hiki cha mapinduzi ya viwanda,nyingine ni kutoa ajira kwa vijana, na pia ni chanzo cha Mapato cha Halmashauri.
Kiwanda hiki kikikamilika kitasaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha kupungua kwa mvua, ukosefu wa rutuba katika udongo, pamoja na matatizo mengine ya Mazingira.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.