Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh.Daniel Chongolo, alipokuwa mwenyekiti katika kikao cha kamati ya Afya ya msingi kilichofanyika leo kwa lengo la kupitia na kujadili maswala ya msingi ya utekelezaji wa huduma za afya, ikiwemo utekelezaji wa kampeni ya ugawaji dawa kingatiba kwa magonjwa ya mabusha na matede.
Amesema katika kampeni hii inayotarajia kuanza tarehe 15/12/2018 hadi tarehe 20/12/2018, Kinondoni kwa kushirikiana na Wizara ya Afya maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto, kupitia kitengo cha magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, imelenga kufikia wananchi takribani milioni 1.2, katika kata zake 20, na mitaa 106.
"Kwanza niseme tunaishukuru Serikali kupitia kitengo husika cha kampeni hii, kwani ,Taifa lenye tija, ni taifa la watu wenye afya bora, hivyo hatuna budi sisi kama kamati kuhakikisha wananchi wanahamasika na wanajitokeza kwa wingi kupata kingatiba hii, na hii itatokana na elimu madhubuti itakayotolewa nanyi, kwa njia zilizosahihi na kuwafikia wananchi kwa usahihi na wakati"Amesisitiza Chongolo
Akieleza hatua zilizochukuliwa hadi sasa kuhusiana na kampeni hiyo, Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele katika Manispaa hiyo, Dr.Neema Mlole amesema wagawa dawa takribani 392, wanaotakiwa kugawa dawa za kinga wameshapatiwa mafunzo, zoezi la ugawaji dawa za kingatiba za kuzuia magonjwa ya kichocho na minyoo kwa ngazi ya Wilaya zimeshafanyika, usambazaji wa dawa na vifaa maalumu umeshafanyika, pamoja na kufanyika kwa maandalizi mazuri ya usimamizi wa zoezi zima.
Katika hatua nyingine mratibu wa zoezi la lishe Manispaa ya Kinondoni Bi Emiliana Sumaye, alipotakiwa kuzungumzia zoezi hilo amesema lengo ni kutoa huduma jumuishi za kinga bila malipo kwa ajili ya kuimarisha afya ya mtoto na kuyataja mafanikio yake kuwa ni kupata ushirikiano mkubwa kwa timu ya wataalamu juu ya utekelezaji wake na pia kufikia asilimia 102% ya utoaji wa matone ya vitamin A katika vituo vya afya na zahanati.
Aidha Bi Sumaye pia ameainisha changamoto zilizojitokeza katika uendeshaji wa zoezi hilo kuwa ni ufinyu wa bajeti, ukosefu wa vifaa tiba, pamoja na upungufu wa watoa huduma juu ya matibabu ya utapiamlo mkali.
Kamati hiyo iliyohudhuriwa na mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya na wakuu wa idara na vitengo, pia imejadili taarifa za utekelezaji wa zoezi la utoaji wa kingatiba za magonjwa ya matende na mabusha na taarifa ya utekelezaji wa zoezi la mwezi lishe la utoaji wa Vitamin A.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na habari.
Manispaa ya kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.