Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi ameeleza kuwa Manispaa ya Kinondoni imeandaa mpango makakati wa kupima ardhi na mashamba yote yanayomilikiwa na umma na wananchi binafsi ili kuwezesha ardhi yote kuwa na hati na kuweka mpango bora wa matumizi unaozingatia uwepo wa huduma za jamii.
Akieleza uamuzi huo Hapi amebainisha kuwa mkakati huo unalenga kumaliza kabisa migogoro ya Ardhi Wilayani humo na kwamba wamiliki wa mashamba wasioweza kumudu gharama za upimaji watalazimika kuingia makubaliano maalum na Manispaa hiyo ili kulipia gharama hizo kwa mtindo wa kugawana idadi ya viwanja baada ya upimaji.Viwanja vitakavyogawiwa kwa Manispaa vitauzwa kwa wananchi wengine ili kulipia gharama za upimaji wa Ardhi.
Aidha amewataka wavamizi wote wa maeneo ya wazi kuacha mara moja kufanya uhalifu huo kwani ni kinyume cha sheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Ametoa kauli hizo leo, alipokuwa akizungumnza na watendaji na viongozi wa Kata ya Wazo, katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo pamoja na utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Kinondoni.
Amesema migogoro mingi ya ardhi husababishwa na ardhi kutopimwa na hivyo kuchochea uvamizi na ujenzi holela usiozingatia sheria.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ameyataja maeneo yanayoongoza kwa uvamizi kuwa ni Kata za Mabwepande, Bunju, na Wazo ambako baadhi ya wananchi wanamiliki mashamba makubwa ambayo hayajaendelezwa.
Hii ni Kata ya Tano kati ya Kata kumi za awamu ya pili ya ziara yake katika Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.