Wilaya ya Kinondoni inaendelea kutekeleza mkakati wa kuviboresha na kujenga vituo vya kutolea huduma za Afya ili viweze kutoa huduma bora inayoendana na mahitaji halisi ya wananchi. Mkakati wa uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za Afya ni malengo mahsusi ya Mpango Mkakati wanne(iv) wa sekta ya Afya (HSSP-IV) na pia ni moja ya lengo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 Ibara ya 50(a) (i).
Katika utekelezaji wa mpango huu, Wilaya ya Kinondoni ilinunua majengo ya kilichokuwa Kituo cha kulelea watoto cha Dogo Dogo Center kilichopo Kata ya Kigogo mwezi Desemba 2017 kwa gharama ya Shilingi Million Mia Nne (Shilingi 400,000,000.00) na kufanya ukarabati wa majengo ya zamani kwa gharama ya shilingi Milioni Hamsini na Nne laki Nne Thelathini na Nne Elfu mia Nane na Tatu (Shilingi 54,434,803) pamoja na ujenzi wa jengo jipya na miundombinu yake kwa gharama ya shilingi Milioni Mia Tano Hamsini (Shilingi 550,000,000) kati yake 400,000,000.00 zikiwa zimetolewa na OR-TAMISEMI na 150,000,000.00 vyanzo vya ndani vya Manispaa (Own Source).
Kwa mujibu wa makadirio ya gharama za ujenzi ambao unahusisha ukarabati wa majengo ya zamani, ukarabati uzio na ujenzi wa majengo mapya kiasi cha fedha Shilingi Milioni Mia Saba Arobaini Laki Tano Sitini na Mbili Elfu Mia Tano (shilingi 740,562,500). Gharama hizi hazihusishi ununuzi wa vifaa tiba, lifti ya kupandia na generator ya umeme wa dharula.Mfumo ambao unatumika katika ujenzi wa jengo hili ni “Force Account”. Mfumo wa “Force Account” ni utekelezaji wa agizo la OR-TAMISEMI katika ukarabati au ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za Afya nchini, ili kupunguza gharama na kuongeza ubora wa majengo yatakayojengwa.
Kituo cha Afya Kigogo kinatarajia kutoa huduma kwa wananchi wa Kata ya Kigogo wapatao 70,288 pamoja na wananchi wa Kata nyingine za jirani zinazojumuisha huduma za wagonjwa wa kutwa (OPD), wagonjwa wa kulazwa (IPD), huduma za maabara, huduma za macho, Afya ya uzazi na mtoto (Reproductive and Child Health), huduma za upasuaji, huduma za ushauri nasaha na kupima Virusi vya Ukimwi (VCT).
Kituo hicho kitakuwa Kituo cha Afya pekee katika Manispaa ya Kinondoni chenye uwezo wa kutoa huduma za kulaza wagonjwa na huduma za upasuaji, hivyo kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda Hospital ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala na kupunguza vifo vya akina mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.Kituo cha Afya Kigogo kinatarajiwa kuanza kutoa huduma kwa wananchi kuanzia tarehe 01 Oktoba baada ya kupata usajili na bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba toka bajeti ya mwaka 2019/2020.
PICHA YA MRADI WA UJENZI WA JENGO JIPYA KITUO CHA AFYA KIGOGO GHOROFA NNE (WODI YA WATOTO, WODI YA KINA MAMA, WODI YA UPASUAJI NA MAABARA) MRADI WA UJENZI NA UKARABATI WA KITUO CHA AFYA KIGOGO
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.