Kituo cha kilimo Malolo chenye jumla ya hekari 45 kinapatikana katika Kata ya Mabwepande jijini Dar es Salaam kinamilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na ni mahsusi ili kuwawezesha wananchi kupata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali kuhusu kilimo, mifugo na usindikaji.
Mafunzo ya kilimo cha kisasa, umwagiliaji wa matone, matumizi ya neti maalum za kilimo pamoja na masoko hutolewa bure kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wengine ambao ni wakazi katika Manispaa ya Kinondoni.
Mazao yanayolimwa katika Kituo cha kilimo Malolo ni Alizeti, ndizi, mazao ya mbogamboga ikiwemo mchicha, majani ya maboga, matembele, sukuma wiki, biringanya, majani ya kunde n.k.
Mboga za matunda zinazolimwa katika Kituo cha Malolo ni pamoja nyanya, pilipili, pilipili hoho, maembe, mapapai, matikiti maji, matango pori na machungwa. Mahindi mabichi pia yanalimwa katika Kituo cha kilimo Malolo kama zao la biashara.
Wakulima pia wanapata fursa ya kufundishwa matumizi ya kitalu nyumba ambayo hutumika katika kuboresha mazingira ya ukuaji wa mimea hususan kupunguza joto kali kutokana mionzi ya jua pamoja na kutunza unyevunyevu katika udongo. Neti maalum za kilimo hutumika katika kitalu nyumba ili kupunguza mwanga mkali wa jua pamoja na kuzuia wadudu waharibifu kwenye mimea.
Umwagiliaji wa matone ni aina ya umwagiliaji ambayo hutumia mipira maalumu yenye matundu au isiyo na matundu, ambapo mtumiaji ataitoboa kulingana na nafasi ya zao husika. Maji hutolewa kwa mfano wa dripu katika kila shina ama penye tundu. Mfumo huu wa kisasa wa umwagiliaji mimea hasa mazao humwezesha mkulima kulima kipindi chote cha mwaka pasipo kutegemea mvua, kumwongozea uzalishaji wa mazao pamoja pato la mkulima na pato la taifa kwa ujumla.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.