Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imepokea wageni kutoka Jiji la Mwanza wakiwemo Waheshimiwa Madiwani na Watendaji wakiongozwa na Naibu Meya wake Mhe. Bhiku Kotecha kwa ajili ya ziara ya mafunzo na kuimarisha mahusiano ambapo walitembelea miradi mitatu ya ufukwe wa Oysterbay (Coco beach), stendi ya daladala Mwenge na uwanja wa mpira wa miguu Mwenge.
Akiwakaribisha wageni hao kwa niaba ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Samson Joseph Rwegasira aliwataka wajisikie huru kujifunza kwa kuuliza waliyonayo ili waweze kutimiza malengo yaliyokusudiwa ya ziara yao ikiwa ni pamoja na kupata mwongozo wa juu ya utekelezaji endelevu wa miradi ya kimkakati ndani ya Manispaa ya Kinondoni.
Ziara hiyo ilitanguliwa na mawasilisho ya taarifa maalumu kuhusu mpango mkakati wa Manispaa ya Kinondoni kuibua vyanzo vya mapato kupitia miradi mbalimbali iliyowasilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Fedha, ndg. Onesmo Mwonga.
Mwisho wajumbe wote wa ziara hiyo ya mafunzo kutoka Jiji la Mwanza waliuliza maswali na kupata majibu na ufafanuzi kutoka kwa timu ya wataalamu ya Manispaa ya Kinondoni na kuridhishwa na jinsi Manispaa ya Kinondoni ilivyojipanga katika eneo la kuibua vyanzo vya mapato. Kisha wakaishukuru Manispaa ya Kinondoni kwa ushirikiano waliopewa na kuwezesha kufanikisha malengo ya ziara yao na kuomba ushirikiano huo udumishwe kwa manufaa ya pande zote.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.