KUHAKIKISHA WANASHIRIKIANA NA NIDA WILAYANI HAPO, KUWASAJILI KATIKA DAFTARI LA TAIFA NA KUWATAMBUA KWA LENGO LA KUPATIWA VITAMBULISHO VYA TAIFA.
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Daniel Chongolo, alipokuwa mgeni rasmi kwenye zoezi la usajili na utambuzi wa watu wenye ulemavu kwenye daftari la Taifa, lililofanywa na NIDA, kwa kushirikiana na SHIVYAWATA, pamoja na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Manispaa ya Kinondoni, kwa lengo la kupatiwa vitambulisho vya Taifa.
Amesema zoezi hili ni zuri, kwani kwa kufanya hivi ni kutekeleza haki ya msingi kikatiba na pia ni kutoa fursa ya watu wenye ulemavu kusajiliwa na kupatiwa vitambulisho vya Taifa, na kuwataka wananchi wanaoishi nao majumbani, kuhakikisha wanawaleta kwa ajili ya zoezi hilo la siku tatu la utambuzi na uandikishaji linaloendelea katika shule ya Ndugumbi Manispaa ya Kinondoni.
"Wito wangu kwa wanakinondoni, wito wangu kwa wale wanaoishi na watu wenye ulemavu, naomba sana ndani ya siku tatu hizi, muwashawishi, wawalete, wawape fursa watu wenye ulemavu kutumia haki yao ya msingi waliyopewa ya kujisajili kwenye daftari la Taifa, kwa ajili ya kupata vitambulisho vya Taifa".Amesisitiza Chongolo.
Awali akitoa taarifa ya zoezi hilo, Afisa Msajili wa NIDA Wilaya ya Kinondoni Ndg. Dickson Mmbaga amesema, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Kinondoni kupitia zoezi hili tumetambua, tumesajili, tumeweka mazingira wezeshi na kupata takwimu zitakazosaidia kuboresha maendeleo ya watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kupatiwa vitambulisho vya Taifa vitakavyowasaidia katika shughuli zao mbalimbali.
Aidha amezitaja faida za kupatiwa vitambulisho vya Taifa kuwa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma zote za msingi, kumtambulisha mtu mwenye ulemavu anapohitaji huduma, kumuwezesha kujidhamini kama anahitajika kufanya hivyo, kurahisisha zoezi la kuhesabu watu, pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa watu wenye ulemavu.
Naye Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Wilaya ya Kinondoni, Bi.Subira Semsimbazi alipokuwa akitoa salaam za shukrani kwa Mkuu huyo wa Wilaya, ameainisha changamoto zinazowakabili kuwa ni ukosefu wa ofisi, ukosefu wa wakalimani, kutopatiwa huduma za bima afya, na pia kutopatiwa mikopo ya wanawake na vijana ili waweze kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali.
Zoezi hili la utambuzi na usajili wa watu wenye ulemavu kwenye daftari la Taifa, kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya Taifa linafanyika kwa siku tatu katika shule ya msingi Ndugumbi iliyoko Manispaa ya Kinondoni.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.