NI KWA LENGO LA KUHAKIKISHA UTARATIBU UNAFUATWA KATIKA KUENDESHA BIASHARA HIZO NA HALMASHAURI KUKUSANYA MAPATO YAKE.
Wiki mbili zimetolewa kwa Wamiliki wa vibanda vilivyopo katika soko la Tegeta nyuki kuhakikisha wanaingia mikataba na Halmashauri ili waweze kufanya Biashara zao na pia mapato yaweze kukusanywa.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Alli Hapi alipokuwa akiongea na wafanyabiashara hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo viwanja vya Manispaa.
Amesema kwa muda mrefu sasa wamiliki hao wa vibanda wamekuwa wakipangisha vibanda hivyo,kwa wafanyabiashara wengine kinyume cha utaratibu na kujipatia kipato kikubwa huku wakiilipa Manispaa kiasi kidogo Cha fedha.
" leo hii tunapeleka miundombinu pale, hizo fedha zinarudije wakati mtu anampangisha mtu kwa tsh 150,000/=, alafu Halmashauri inapata tsh 21,000/=haiwezekani, hii lazima ifike mwisho, na mwisho wake ni mmoja tu, kama huna mkataba na mwenyemali tafsiri yake wewe ni mvamizi, anayefanya biashara aingie mkataba na Halmashauri mmiliki, kwa sababu wengi wenu mmekaa zaidi ya miaka kumi pale, hata kama ulijenga kibanda chako ndani ya miaka kumi umesharudisha fedha zako, halmashauri inapata 21,000/="Amebainisha Hapi.
Ameongeza kuwa imefika muda Sasa kwa Serikali kusimamia maeneo yake ya soko ili iweze kukusanya mapato yatakayowezesha kuboresha huduma nyingine za kiuchumi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndg Maduhu Kazi amesema, watafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na mikataba itaandaliwa ili wamiliki hao wa frem waweze kufanya biashara zao na serikali iweze kujipatia mapato.
Kwa upande wao wamiliki wa vibanda hivyo wamekubaliana kwa kauli moja kushirikiana na serikali katika kuingia mikataba, kwenye maeneo hayo ili waweze kufanya biashara zao kwa amani.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.