Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tawala wa Wilaya na Mameya wa Halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam kuwa na mikakati madhubuti na mbinu mbadala na endelevu kwa lengo la kuhakikisha Jiji linakuwa safi muda wote usiku na mchana.
RC Chalamila amesema hayo leo Juni 05, 2023 katika kilele cha Siku ya Mazingira Duniani ambayo huadhimishwa tarehe 05 Juni kila mwaka na kwa Mkoa wa Dar es Salaam imeadhimishwa katika Wilaya ya Kinondoni iliyoenda sambamba na kauli mbiu isemayo: "Pinga Uchafuzi wa Mazingira Unaosababishwa na Taka za Plastiki".
"Niwaombe Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tawala Wilaya na Mameya wote kutoka Wilaya zote tano za Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanaweka mikakati madhubuti na mbinu zilizo bora na endelevu katika kuhakikisha Jiji letu linakuwa safi muda wote na sio mchana tu", Amesema Mhe. Chalamila.
Pia, Mhe. Chalamila amesisitiza suala la kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki na kutumia vifungashio mbadala. "Dar es Salaam ina matumizi makubwa ya mifuko ya plastiki katika uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa plastiki hivyo elimu itolewe na kuacha matumizi hayo".
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewaagiza Wakurugenzi wote kuwa na vitalu vya uzalishaji miti, maua na vingine vitakavyoweza kupendezesha mji wa Dar es Salaam kwani uchafu unaozalishwa na taka katika mji huu sasa ni fursa kwa vijana wengi kama ambavyo taasisi na vikundi mbalimbali vimekuwa vikijikita katika kutengeneza fursa kupitia taka.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule amesema suala la utunzaji wa mazingira lipo vizuri Kinondoni na utunzaji wa mazingira unatakiwa uanzie ngazi ya familia.
"Kila mmoja anapaswa ajue jinsi ya kuhifadhi na ajue sehemu ya kupeleka taka ikiwemo matumizi sahihi ya taka zinazooza ili ziwe na manufaa kama mbolea na chakula cha mifugo na sio kuziharibu pasipo kujua faida zake", Amesema Mhe. Saad.
Maadhimisho hayo kimkoa yamefanyika katika Kata ya Makumbusho iliyopo Wilaya ya Kinondoni.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.