Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, amemtaka Mkandarasi Hinan International kukamilisha kwa haraka ujenzi wa mradi wa kituo kipya cha mabasi madogo kilichopo Mwenge Manispaa ya Kinondoni.
Akiwa katika ziara ya siku moja Julai 11, 2022 ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi wa Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Majaliwa alieleza kuwa ukamilishaji wa mradi huo utawawezesha wafanyabiashara wa eneo hilo kuendelea na shughuli zao huku Manispaa ikiendelea kukusanya mapato. “Ujenzi wa stendi ukamilike kwa wakati ifikapo Februari, 2023 ili wafanyabiashara waliosajiliwa warejee kwenye shughuli zao,” alisema Mhe. Majaliwa.
Katika ziara hiyo Waziri Mkuu pia alikagua mradi wa ujenzi wa uwanja wa mpira uliopo jirani na stendi hiyo.
Aidha Mhe. Majaliwa amewataka wakazi wa mtaa wa Tandale kwa Mtogole kuhakikisha wanatunza mazingira ya mto Ng’ombe ili kuepukana na uchafuzi wa mazingira.
Aliyasema hayo wakati alipotembelea eneo hilo ambapo pia amewahakikishia wananchi wa eneo hilo kuwa kipande cha barabara kisichokuwa na lami kitawekewa lami, taa pamoja na kuboresha mazingira ya eneo la Mtaa wa Uwanja wa Fisi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Majaliwa amewataka watumishi wa Manispaa ya Kinondoni kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu, uwajibikaji na utendaji wenye kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Amesisitiza kwa Wakuu wa Idara kutembelea wananchi kwa lengo la kusikiliza kero, kutolea ufafanuzi wa masuala mbalimbali na kupata mrejesho wa maoni ya wananchi.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.