Wazee waishio Wilaya ya Kinondoni wametakiwa kufuatwa kwenye Kata, Mitaa na maeneo wanayoishi ili waweze kutambuliwa kwa lengo la kupatiwa kadi za msamaha wa matibabu.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Ali Hapi alipozuru katika kata ya Wazo na kukutana na wananchi wa mtaa wa kilimahewa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanjani hapo.
Amesema lengo la ziara yake ni ya kiserikali na kikazi pia, yenye nia ya kukutana na wananchi wa eneo husika kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
"Nimepewa kazi na Mh Rais, kwa hiyo nafanya kazi, hivyo niko hapa kama mtumishi wenu, ninyi ndio mabosi, Watendaji wanapaswa kujua kwamba ninyi wananchi ndio mmewaajiri na wanapaswa kutatua matatizo yenu, viongozi hatupaswi kuwa sehemu ya kutengeneza matatizo, viongozi tunapaswa kuwa sehemu ya suluhu ya matatizo,huo ndio uongozi bora ,na nilishasema tokeni ofisini, Mtendaji wa Kata, maafisa ugani wa kata watendaji wa Mitaa, tokeni ofisini nendeni kwa wananchi makasikilize shida zao ili muweze kuwapa maelezo na mipango ya Serikali kuhusiana na maeneo yao"amesisitiza Hapi
Amefafanua kuwa yapo mambo mengi ambayo Serikali imeyatilia mkazo hasa swala la matibabu ya bure kwa wazee na utekelezaji wake unaendelea vizuri.
"Nimewaagiza watendaji wangu, wafuateni wazee kwenye Kata na Mitaa yao, ili muweze kuwatambua, na kuwapatia kadi za msamaha wa matibabu, Serikali yetu imekwishasema wazee pamoja na watoto chini ya umri wa miaka mitano matibabu kwao ni bure, na hilo sina wasiwasi nalo kwa kuwa najua linatekelezeka "amesema Hapi
Amefafanua kuwa wazee ni hazina pekee tuliyonayo na hasa ikizingatiwa wameitumikia nchi yetu kwa kipindi chote hicho, hivyo yawapasa kutibiwa bure na hata wakati mwingine wasipange foleni.
Katika hatua nyingine amewataka wanachi kushirikisha Serikali pale inapotokea kuwepo na michango isiyoeleweka, isiyofuata utaratibu, wala kanuni za fedha ili matapeli hawa waweze kukomeshwa.
"Kuchangia maendeleo ni jambo zuri sana, na sisi tunahamasisha wananchi kuchangia maendeleo, lakini michango inautaratibu wake, nawaomba Sana pale mnapotaka kuchangia Jambo lenye nia ya maendeleo, washirikisheni viongozi wenu wa Serikali ili tujue na turizike, na wakati mwingine tujiridhishe kwamba lile mnalotaka kulichangia haliko kwenye mpango wa Serikali wa karibuni katika kulitekeleza "Amebainisha Hapi
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.