Wazazi na Walezi kutoka Kata ya Bunju, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wametakiwa kuzingatia vyakula vyenye makundi matano wakati wa uandaaji wa vyakula kwa watoto wao.
Hayo yamebainishwa na Afisa Lishe kutoka Sehemu ya Kilimo na Mifugo Manispaa ya Kinondoni Bi. Luciana Msangi wakati akitoa mafunzo ya lishe na namna ya uandaaji wa chakula hivyo kwa vitendo Disemba 22, 2023 katika Ofisi ya Mtendaji Kata ya Bunju.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Kata ya Bunju ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Mkataba uliosainiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na maelekeo ya Mkurugenzi wa Manispa ya Kinondoni Bi. Hanifa Suleiman Hamza, kwamba kila Kata inapaswa kutoa mafunzo ya lishe kila baada ya miezi mitatu.
"Leo tupo Kata ya Bunju kutoa mafunzo ya lishe na namna ya uandaaji wa vyakula vinavyozingatia makundi matano ya vyakula kama vile vyakula vya mizizi, nafaka, mafuta, mbogamboga na matunda ili kuisaidia jamii kuwa na kizazi chenye afya bora kwani vyakula hivi vinasaidia kuondokana na magonjwa nyemelezi yasiyoambukiza pamoja na ukuaji mzuri wa watoto," amesema Bi. Luciana.
Aidha Bi. Luciana amewashauri akina mama hao kuwa makini wanapoandaa vyakula vya lishe kwa watoto wao hasa uandaaji wa uji wa lishe wenye mchanganyiko wa nafaka zaidi ya moja ambapo kwa wamama wenye watoto kuanzia miezi 6 wanatakiwa kitumia chakula chenye nafaka aina moja tu kwani mfumo wao wa chakula unakuwa bado hauwezi kumeng'enya mchanganyiko wa vitu vingi.
Lakini pia Bi. Luciana ameshauri kuwa watoto wenye umri kuanzia mwaka mmoja na kuendelea wanatakiwa kupewa chakula chenye mchanganyiko wa aina zisizozidi mbili pamoja na kuongeza virutubishi kama karanga, maziwa, mbegu za maboga wakati wa kupika uji na sio kuvisaga pamoja kama wengi walivyozoea kwani kufanya hivyo wanatengeneza sumu kavu ambayo sio nzuri kwa watoto bila ya kusahau matunda na mbogamboga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wenyeviti Wilaya ya Kinondoni Bw. Lazarious Mwakiposa amewasisitiza wamama hao kutokuwa wavivu katika uandaaji wa vyakula ndani ya familia zao ili kuondokana na magonjwa hatarishi yanayosababishwa ulaji usiofaa hasa kwa watoto wao.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.