NI KATIKA KUHAKIKISHA WANAKUWA KWENYE NAFASI NZURI YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZINAZOWEZA KUJITOKEZA WAKATI WA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO YA KAZI.
Watumishi wa sekta ya Afya kote Nchini wametakiwa kuhakikisha wanaacha mazoea na kufanya majukumu yao kwa weledi kwa kufuata kanuni zote za afya wakati wa kumuhudumia mgonjwa, ili waweze kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Kauli hiyo imetolewa leo na Afisa Afya Manispaa ya Kinondoni Bw John Kijumbe wakati wa kufungua mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo watumishi wa afya wa jinsi ya kujikinga na maambukizi wanayoweza kuyapata wakati wanatekeleza majukumu yao.
Amesema sekta ya Afya ni eneo muhimu Sana linalohitaji umakini na usahihi mkubwa hivyo watumishi wake wanatakiwa kuhakikisha wanazingatia misingi yao ya kazi na umakini mkubwa utakaowasaidia si tu kujiepusha na mambukizi, bali kutenda haki na wajibu kwa mgonjwa anayepatiwa matibabu.
Ameongeza kuwa yapo magonjwa ambayo mtumishi wa Afya anahitaji umakini wa kutosha wakati wa kumuhudumia mgonjwa, na kuyataja magonjwa hayo kuwa ni magonjwa ya kuharisha, kuharisha damu, homa ya matumbo na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Naye mratibu wa Mafunzo hayo Bi Rose Temu ameiomba Serikali kuweka miundombinu mizuri na iliyorafiki itakayomwezesha mtumishi wa sekta ya afya kutekeleza majukumu yake kwa usahihi anapokuwa katika eneo lake la Kazi ili kuweza kuepukana na maambukizi ya maradhi yanayoweza kujitokeza.
Mafunzo hayo yamefadhiliwa na shirika la Japan la JICA, yenye lengo la kuwajengea uwezo watumishi wa sekta ya Afya wa jinsi ya kujikinga na maambukizi wakati wa kutekeleza majukumu yao, na umuhimu wa kuzijua njia kumi za kunawa mikono kwa usahihi.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.