Wazazi na walezi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wakumbushwa kuwasaidia na kutatua changamoto za watoto wa kike ili waweze kufikia ndoto zao.
Hayo yamebainishwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kinondoni Bi. Zena Nalipa katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike yaliyofanyika katika uwanja wa shule ya Msingi Bunju A uliopo Kata ya Bunju Manispaa ya Kinondoni.
“Niwaombe wazazi na walezi wote ndani ya Manispaa ya Kinondoni kupitia siku hii wawe mstari wa mbele katika kuwasaidia na kutatua changamoto ambazo zimekuwa chanzo cha ukatili wa kijinsia kwa watoto wao wa kike kwani kufanya hivyo itawasaidia sana watoto wa kike kutimiza malengo na ndoto zao hasa katika nyanja za kiuongozi,” amesema Bi. Zena.
Lakini pia Bi. Zena amewaomba watoto wa kike kutokaa kimya pindi wanapoona wanafanyiwa aina yoyote ya ukatili wa kijinsia kwani Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imejipanga vizuri katika kuhakikisha wanakomesha vitendo vyote vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa watoto.
Katika kuhakikisha hilo Afisa Maendeleo ya Jamii huyo amesema ndani ya Manispaa ya Kinondoni tayari imeshajipanga kwa kuanzisha madawati ya jinsia katika maeneo mbalimbali, hivyo endapo mtu yeyote atafanyiwa ukatili basi afike bila kusita.
Mmoja wa watoto wa kike na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Bunju A, Kiza Khamis ameishukuru Manispaa ya Kinondoni kwa kuendelea kuadhimisha siku hiyo ya mtoto wa kike kwani imekuwa ikiwasaidia kukumbushana mambo mbalimbali na kupata ufumbuzi wa mambo yao ambayo yanakuwa kikwazo cha kufikia malengo yao.
Mbali na hayo pia mwanafunzi huyo ameiomba Serikali kuendelea kuunda mabaraza mbalimbali ambayo yatashughulika na kupambana na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wa kike wote nchini ili waweze kutimiza ndoto zao na kulisaidia taifa letu maana vijana ndio taifa la kesho.
Ikumbukwe kuwa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 11 ya mwezi wa 10 kila mwaka ambapo mwaka huu yameenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Haki Zetu ni Hatma Yetu: Wakati ni Sasa”.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.