NI KUTOKANA NA KUSHUKA KWA KIWANGO CHA UNAWAJI WA MIKONO KWA USAHIHI KUTUMIA SABUNI NA MAJI YANAYOTIRIRIKA.
Watoto takribani milioni 3.5 kote uliwenguni hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu, na hii ni kutokana na kutokunawa mikono kwa usahihi.
Hayo yamebainishwa leo na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tandale Sokoni Bi. Murshda Ally Kiswela alipokuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Diwani wa Kata hiyo, kwenye mkutano wa mafunzo ya kuongeza uelewa juu ya kuzuia na kujikinga na maambukizi ya magonjwa kwa unawaji sahihi wa mikono, uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi tandale.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea watanzania hasa wanafunzi, uwezo na uelewa wa jinsi gani mikono inatakiwa kuoshwa, na kuhakikisha inabaki safi na salama ili kujiepusha na magonjwa hatarishi ya mlipuko yatokanyo na unawaji usio sahihi.
"Lengo la mkutano huu wa mafunzo ni kuwajengea uelewa na ufahamu zaidi wa umuhimu wa unawaji mikono kwa kupitia njia kumi kwa maji tiririka na sabuni, na kukausha mikono kwa kitambaa kisafi au tishu ,hii ni njia madhubuti na rahisi katika udhibiti wa magonjwa yanayoweza kusababishwa na mikono iliyochafuka na vimelea vya magonjwa, inadaiwa kwamba magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu yanatokana na unawaji wa mikono usio sahihi, takribani watoto milioni 3.5 waliochini ya miaka mitano hupoteza maisha kila mwaka duniani kote. "Ameeleza Mwenyekiti
Naye Dr. Omary Mwangaza ambaye ni mganga mfawidhi wa kituo cha Afya Magomeni amebainisha kuwa kila siku duniani watoto takribani elfu mbili mia moja tisini na tano(2,195) hupoteza maisha kwa ugonjwa wa kuharisha, na watoto takribani laki mbili na nusu, (250,000), hupoteza maisha kwa ugonjwa wa kipindupindu.
Amesema asilimia hamsini ya magonjwa hayo yanayosababishwa na kutokunawa mikono katika jamii ikiwa ni pamoja na kipindupindu, kuhara, kutapika, kuharisha damu, pamoja na Amoeba yatapunguwa endapo njia sahihi za unawaji wa mikono zitafundishwa, kuzingatiwa na kudumishwa.
Kadhalika Afisa Afya wa Manispaa hiyo Ngd John Kijumbe ameongeza kuwa Manispaa ya Kinondoni ili kuondokana na magonjwa yanayosababishwa na unawaji wa mikono usio sahihi imepanga kuweka progam pamoja na bajeti ya kutosha kwa idara na vitengo vyote ili iweze kutoa elimu ya unawaji wa mikono kila kata na mashuleni kwa wakati na usahihi.
Katika hatua nyingine Sr. Rose Temu ambaye ni Afisa Muuguzi kituo cha Afya Magomeni ameainisha njia kumi sahihi za unawaji wa mikono kuwa ni kwanza kulowanisha mikono kwa Maji, weka sabuni ya kutosha kiganjani, sugua kiganja kwa kiganja, osha nyuma ya kiganja na safisha vidole kwa kupitanisha.
Nyingine ni safisha nyuma ya vidole kwa kukunja vidole, safisha vidole gumba, safisha kucha za mkono mmoja mmoja kwenye kiganja cha mkono mwingine, suuza mikono kwa maji safi, kausha mikono kwa karatasi au kitambaa kisafi, na mwisho funga bomba kwa kiwiko au tishu.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano na habari
Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.