Watendaji wa Kata, Mitaa pamoja na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wametakiwa kuwa waadilifu katika utendaji wao ili kuepukana na migogoro isiyoyalazima inayoweza kujitokeza katika utendaji wao wa Kazi.
Agizo hilo limetolewa na Mstahiki Meya Manispaa ya Kinondoni Mh Benjamin Sitta alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya Utawala bora yaliyoratibiwa na Mkoa kwa Watendaji wa Kata, Mitaa pamoja na Wenyeviti yaliyofanyika katika ukumbi wa Kingsolomon.
Amesema mafunzo haya ni muhimu kwa ngazi hizi za chini kwani yatasaidia kupunguza malalamiko yanayojitokeza kwa wananchi hasa ikizingatiwa yamekuwa mengi, na hii ni kutokana na kutokuwajibika, kutokufika ofisini kwa wakati, na kutotimiza majukumu kwa wakati.
"Sasa kunawatendaji wazuri na watendaji wabaya, na nikatoa mfano juzi tumemfukuza Mtendaji mmoja, kwa sababu ya uzembe wa kutotokea kazini na sisi hatuna msamaha katika hilo. "Amesisitiza Meya
Amesema lengo kuu ni kukumbushana, kuelekezana, sheria, miongozo, kanuni na wajibu katika kutekeleza majukumu yao.
"kwa hiyo tunachofurahia mafunzo haya ya siku Mbili kwanza yatawakumbusha sheria, kanuni na miongozo, yatawakumbusha wajibu wao, yatawakumbusha kwanini wako pale. "Amesisitiza Sitta.
Naye Bi Mary Assey ambaye ni katibu tawala Msaidizi ofisi ya Mkuu wa Mkoa amesema mafunzo haya ni kufuatia Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam iliyofanyika mwezi Novemba iliyojulikana kwa jina la "Dar Mpya " na kugundua changamoto nyingi zilizojitokeza ni kuhusiana na uelewa mdogo walionao watendaji wetu kwenye maswala ya utawala bora.
Amesem lengo kubwa ni kumsaidia Mtendaji wa Kata na Mtaa pamoja na Mwenyekiti kuhakikisha anasimama kwenye nafasi yake katika kutatua kero na migogoro ya wananchi.
Amezitaja mada zitakazofundishwa katika mafunzo haya ya siku mbili kuwa ni Maswala ya utawala bora, Ulinzi na usalama, Sheria na taratibu za utendaji katika ngazi ya Kata na Mitaa pamoja na Uhamiaji haramu.
Mada nyingine ni Sheria za Mazingira, Usafi wa Mazingira, Sera, Sheria,Kanuni na Miongozo ya Maji pamoja na Usimamizi wa Maswala ya Ardhi.
Mafunzo haya yataendeshwa kwa siku Mbili ambapo mwisho wa siku watatakiwa kupimwa kama la kilichofundishwa kimeeleweka na kinaenda kutekelezwa.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.