Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amewaasa Watanzania kuielewa na kuizingatia falsafa ya 4R iliyoasisiwa na kutumiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa majukumu yetu ili kuyafikia mafanikio na kuwa na maendeleo endelevu.
Hayo ameyasema katika hotuba ya ufunguzi wa kongamano/mdahalo wa kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa Manispaa ya Kinondoni.
Akifafanua falsafa hiyo ya 4R alisema inahusu mambo manne ya msingi ya kuzingatiwa ambayo ni Maridhiano , Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi mpya (Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuilding).
Kuhusu Maridhiano (Reconciliation) alitaka kuhimizwa umoja na amani katika Taifa kwa kuhuisha moyo wa kitaifa na kuinganisha nguvu ya pamoja katika kuleta maendeleo.
Alisisitiza umuhimu wa kuachana na migogoro na mifarakano na kutembea pamoja na kufika pamoja katika safari ya kuleta maendeleo endelevu ya Taifa letu.
Akizungumzia Ustahimilivu (Resilience) amesisitiza umuhimu wa kuzitumia changamoto kama fursa katika kuleta maendeleo kwani katika dunia ya sasa changamoto haziepukiki kwani ni dunia ya sayansi na teknolojia na lazima tukabiliane na kila changamoto kwa Ustahimilivu.
Kuhusu Mabadiliko (Reforms) aliwataka Watanzania kutokuwa watumwa wa historia na lazima kuwa tayari kwa mabadiliko pale yanapohitajika ili kuyafanya mambo kwenda mbele.
Pia aliwataka Watanzania kuwa tayari kujifunza kutoka nchi na jamii nyingine zilizofanikiwa kama China, Singapore na Thailand.
Akizungumzia dhana ya Ujenzi mpya (Rebuilding) alisisitiza umuhimu wa kujifanyia tathimini kwa kuangalia mapungufu yaliyopo na kuyafanyia kazi na kusonga mbele katika kusukuma maendeleo.
Mwisho alisisitiza kama Taifa ni muhimu kuitumia dhana ya 4R katika kusukuma maendeleo. Alisema kuwa dhana hii inaungatia historia yetu uhalisia na kutupeleka mbele (Historic, Realistic and Futuristic) na kwamba inaunganisha historia ya nchi yetu kwa kulinganisha na hali halisi ya sasa ili kusonga mbele zaidi katika mafanikio.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Gondwin Gondwe alimshukuru Katibu Mkuu huyo kwa kukubali kuwa Mgeni rasmi katika kongamano la kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania katika Wilaya ya Kinondoni na kuelezea mafanikio ya sekta zote yaliyofikiwa na Manispaa kwa miaka 61 ya Uhuru.
Kongamano hilo limehudhuriwa na makundi mbalimbali ya wadau wote wa Manispaa yaliyotanguliwa na shughuli mbalimbali za kijamii yaliyoambatana na mashindano pamoja na washindi kupewa zawadi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.