Watanzania kote nchini wametakiwa kuhakikisha wanakuwa walinzi wakubwa wa mikondo ya maji inayoharibiwa na wachache kwa kujenga kwenye maeneo hayo kinyume cha Sheria na kuzuia maji kunakosababisha mafuriko yanayoleta athari kubwa kipindi cha mvua.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh.Alli Hapi alipofanya ziara kutembelea maeneo ya barabara yaliyoathirika na mvua zinazoendelea kunyesha ikiwemo ile barabara ya Shopers Plaza
Amesema mafuriko hayo yamesababishwa na wananchi kujenga kwenye miundombinu ya kupeleka maji baharini na kusababisha kuzibwa kwa mkondo wa Maji na kuleta mafuriko.
Aidha amewataka wahandisi wa Manispaa kufanya tathmini ya ujenzi wa nyumba zilizojengwa kwenye hifadhi ya barabara na mkondo wa maji na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwapa notisi,ya siku saba ya kuwataka wabomoe Majengo yao kwa gharama zao wenyewe.
"Tumejionea wananchi ambao wamejenga kwenye miundombinu ya kupeleka maji baharini, wananchi wamezuia maji, wananchi wamejenga kwenye mitaro, wananchi wamevamia maeneo ya barabara, hatutotoa senti ya Serikali kwenda kumbomolea mvamizi ambaye amevamia yeye mwenyewe, bila yeye kutulipa fidia, kwa hiyo watu wote hao wabomoe wenyewe maeneo yao, vinginevyo tutawabomolea na watatulipa gharama za kwenda kubomoa kuta zao, kubomoa majengo yao, hatuwezi kuwapa shida wananchi waliowengi kwa sababu ya watu wachache kujenga kwenye maeneo ya mikondo ya maji kinyume cha sheria, " Ameagiza Hapi.
Katika hatua nyingine amewataka wale wote wanaokaa mabondeni na maeneo hatarishi ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba zao maeneo hayo, wahame mara moja ili kuepukana na maafa yanayoweza kujitokeza katika kipindi hiki cha mvua.
"Serikali inatoa RAI kwamba wananchi wahame kwa hiari yao maeneo hatarishi ,waende kwenye maeneo ambako ni salama kwa Maisha yao na familia zao. Kwa kweli hatutarajii kwamba tutapata maafa yeyote kutoka kwa maeneo ambako watu wanajua kabisa kwamba maeneo haya ni hatari "Ametahadharisha Hapi.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.