Wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule za Msingi Manispaa ya Kinondoni, wametakiwa kuwapatia watoto wao chakula cha asubuhi kabla hawajaenda shuleni.
Wito huo umetolewa leo na Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Kinondoni, Mwl. Theresia Kyara, wakati akifungua semina kwa Wenyeviti wa Kamati za shule za Msingi 82 na Maafisa Elimu Kata 20 wa Manispaa ya Kinondoni. Semina hiyo iliyohusu Mwongozo wa Lishe Shuleni imefanyika katika shule ya msingi Kinondoni.
Alisema, "Wazazi na walezi hakikisha mtoto unampatia chakula asubuhi kabla hajaenda shule. Serikali, kupitia nyie wazazi, itampatia chakula cha mchana mtoto."
Amesema si vyema kwa watoto kunywa maji yenye rangi ambayo hayana Afya na badala yake wawapatie matunda. Alisema ili kujikinga na maradhi yasiyo ambukiza ni vyema watoto wakapata lishe katika umri mdogo.
Aidha, Mwl. Kyara alizitaka Kamati hizo za shule kuhakikisha zinadhibiti vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa watoto shuleni. "Kamati za shule mnasimamia kila kitu kuanzia taaluma, lishe, mazingira hata nidhamu, hakikisheni vitendo visivyo vya kimaadili vinadhibitiwa."
Naye Afisa Elimu Msingi anayeshughulikia lishe, Mwl. Martha Kussaga, alizitaka Kamati hizo kushirikiana kwa ukaribu na walimu wakuu kudhibiti usafi wakati wa uandaaji wa vyakula vya wanafunzi.
"Vyakula viandaliwe katika mazingira safi ikiwemo wanafunzi kunawa mikono kwa maji tiririka. Simamieni upatikanaji wa chakula, taarifa za mapato na matumizi ya vyakula ziwe wazi," alisema Mwl. Kussaga.
Aidha alizitaka Kamati hizo kuhakikisha masuala ya lishe yanaingizwa katika mipango ya maendeleo ya Kata.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini: Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.