Wanawake nchini Tanzania wametakiwa kuhakikisha wanazitumia vema fursa zilizopo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kimaendeleo halikadhalika kushiriki katika uchumi wa viwanda.
Rai hiyo imetolewa leo na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la wanawake wa Mkoa wa Dar es salaam lililodhaminiwa na Benki ya CRDB, katika viwanja vya Posta Kijitonyama.
Amesema lengo la Jukwaa hili ni kuwaunganisha wanawake na fursa za kiuchumi, kibiashara,kimaendeleo pamoja na masoko, sambamba na hilo, liwe jukwaa la kuibua matatizo ya wanawake eneo wanapoishi ili yatatuliwe na mwisho wa siku waweze kupata muda mwingi wa kujenga uchumi.
Ameongeza kuwa ni jukwaa kwa ajili ya kuweka mipango madhubuti kwa wanawake wanaojishughulisha na Kilimo ili waweze kuzalisha bidhaa zitakazotumika katika viwanda.
Amesisitiza kuwa "Ni lazima watanzania tutengeneze soko letu wenyewe, tutumie bidhaa zetu wenyewe, tujitosheleze wenyewe kimtaji, kiuchumi na kimasoko ili tuweze kufikia uchumi wa viwanda "
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la kuwawezesha wanawake wa Dar Es Salaam ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh Sophia Mjema amesema Jukwaa hili litashuka mpaka ngazi ya Kata, Mitaa, na Tarafa.
Amesema Mkoa wa Dar Es Salaam umejipanga kuhakikisha mgawanyo wa bidhaa na maeneo kwa wanawake wajasirimali unakuwepo ili kuwapatia fursa zaidi za Kibiashara.
Akitoa takwimu za utekelezaji wa Agizo la Makamu wa Rais la uwanzishwaji wa majukwaa ya kuwawezesha wanawake, Katibu wa Baraza la uwezeshaji wa wananchi Kiuchumi Bi. Bang Issa amesema mpaka sasa Mikoa ishirini na tatu (23), Halmashauri mia moja na tano (105),Kata mia mbili thelathini na sita (236),tayari zimeshaanzisha majukwaa ya wanawake yenye lengo la kujenga na kupeana nguvu, kuwawezesha wanawake kushiriki uchumi wa viwanda.
Jukwaa hili la wanawake Mkoa wa Dar Es Salaam ni jukwaa la ishirini na tatu kuzinduliwa leo, lenye kauli mbiu isemayo "Mwanamke tumia Fursa kushiriki uchumi wa Viwanda "
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.