Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ikiwa mshiriki wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2024 imetakiwa kuwachukulia hatua kali watu wote wanaotiririsha maji taka hovyo yanayopelekea mlipuko wa magonjwa ya mlipuko. Agizo hilo limetolewa leo Juni 5, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Albert Chalamila katika maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mji Mwema Wilaya ya Kigambaoni yenye kauli mbiu isemayo "Urejeshaji wa Ardhi, Ustahimilivu wa Hali ya Jangwa na Ukame".
"Katika kuadhimisha siku hii nitoe rai kwa Wakuu wa Wilaya zote tano za Mkoa wa Dar es Salaam kuwachukulia hatua kali watu wote wenye tabia ya kutiririsha maji taka hasa maji ya vyooni kwani utiririshaji wa maji hayo ni chanzo cha uwepo wa magonjwa hatari ya mlipuko hasa kipindupindu ambacho kinaonekana kuwa tishio kwa Mkoa wetu wa Dar es Salaam," amesema Mhe Chalamila. Aidha Mkuu wa Mkoa huyo amewaomba Wakuu wa Wilaya hao, Wakurugenzi wa Manispaa zote na Waheshimiwa Madiwani kuendelea kuhamasisha usafi sambamba na matumizi ya nishati safi kwenye Wilaya zao ili kuweka mazingira safi na salama wakati wote na kuwa kivutuo cha usafi nchini.
"Katika kuunga mkono kampeni ya matumizi ya nishati safi ya Rais wa Jamhuri ta Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan niwaombe Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Madiwani wote wa Mkoa huu kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu juu ya usafi ambao unaenda sambamba na matumizi ya nishati safi na salama. Katika kufanikisha hilo Mheshimiwa Chalamila ametoa ahadi ya kuwapatua mitungi ya gesi zaidi ya 1,500 kwa akina mama kutoka Wilaya zote ambapo kila Wilaya watapatiwa akina mama wapatao 300.
Mbali na hayo pia Mhe. Chalamila amewataka Wakuu hao kuanzisha mashindano ya usafi kwa kila Wilaya ili kuongeza hamasa na kasi ya usafi muda wote na watakao ibuka kinara wa usafi watapewa zawadi ikiwepo magari ta kufanyia usafi ndani ya Wilaya zao.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.