Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kupitia Divisheni ya Maendeleo ya Jamii imetoa mafunzo ya bajeti kwa wanafunzi kutoka Kata 20 ili kuweza kuona namna ya ushirikishwaji wa watoto katika bajeti za Serikali.
Akiongea katika mafunzo hayo Mratibu wa Dawati la Maendeleo ya Watoto kutoka Manispaa ya Kinondoni Bi. Clara Manasseh amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kutaka watoto waweze kufahamu mambo yanayohusu watoto yanawekwa katika bajeti hivyo kama hayawekwi waweze kuwashauri Madiwani na viongozi wengine ili masuala ya watoto yaweze kushugulikiwa katika bajeti kupitia Baraza la Madiwani.
Pia, Bi.Clara ametoa wito kwa watoto waweze kujikita katika masuala yanayowahusu wao, kutambua haki zao na kuwa na maadili mema katika jamii wanazoishi ili kutengeneza Taifa bora na imara.
Kwa upande wake muwezeshaji kutoka UNA Bw. Lucas Kifyasi ameeleza namna ya vijana wanavyotakiwa kuwajibika na kushiriki katika fursa mbalimbali ili waweze kupata haki zao.
Hata hivyo katika mafunzo hayo Bw. Kifyasi amesema Waheshimiwa Madiwani ndio wahusika wakuu wa kujadili bajeti kwa kuangalia vipaumbele vya wananchi.
Vile vile ametoa elimu kuhusu namna ya kuandaa vipaumbele ambapo vipaumbele hivyo vinaandaliwa kila Kata kulingana na mahali ilipo, idadi ya wananchi wake katika umri wowote huwa na vipaumbele vyake.
Pamoja na kuandaa bajeti lakini kuna muingiliano wa kimahitaji unaopelekea kutokamilika kwa baadhi ya miradi ikiwa ni pamoja na mlipuko wa magonjwa, majanga mbalimbali na upandaji wa bei ya vitu ambapo inakua nje ya bajeti za Serikali.
Nae Mtaalamu Afisa Ulinzi wa Mtoto na Haki za Watoto kutoka Shirika la Save the Children Bw. Alex Enock amesema lengo kubwa ni kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kushiriki katika Kata zao kwenye mipango na bajeti na kuhakikisha inatetea haki zao pia kuzijua fursa za ushiriki wa mawazo yao katika kuboresha bajeti ya Serikali.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini: Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.