Wafanya biashara ndogo ndogo Manispaa ya Kinondoni walipo maeneo yasiyo rasmi wametakiwa kuondoka haraka na kurejea maeneo waliyopangiwa.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe, alipokuwa akizungumza na wakazi wa Mtaa wa Madale, Kata ya Wazo wakati wa zoezi la usafi.
Usafi kwa ngazi ya Manispaa umefanyika Madale, Mnada wa Mbuzi Kunoga "Flamingo."
Mtendaji wa Kata ya Wazo, Bw. Sylvester Ntonja, alisema kuwa Wamachinga waliopo Kisanga licha ya kufanyika kwa vikao vingi baina yao na uongozi wa Kata, wamegoma kurudi eneo lililojengwa na Manispaa.
"Mheshimiwa DAS, pale Kisanga Manispaa imeweka miundombinu yote, lakini Wamachinga hawataki kurudi eneo hilo. Tunaiomba Serikali ya Wilaya itusaidie warudi."
Naye Bi. Msofe aliwapongeza uongozi wa Kata ya Wazo kwa kubuni eneo hilo kuwa mnada na kuwataka kufuata taratibu ili usajiliwe rasmi kama mnada.
Kadhalika Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Jumanne Mtinangi, aliwaomba wafanyabiashara hao wa eneo la mnada wa Flamingo, Madale, kujisajili katika vikundi ili wapate mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Manispaa.
Mnada huo ulioanza takribani mwezi mmoja uliopita unakadiriwa kuwa na Wafanyabiashara ndogo ndogo 300 ambapo unachangia katika mapato ya ndani ya Manispaa kuanzia Oktoba 25, 2022.
Katika kikao cha Mkurugenzi wa Manispaa na Watendaji wa Kata kilichofanyika Novemba, 2022 mwanzoni, Mtendaji wa Kata ya Wazo alikitaarifu kikao hicho kuwa Kata yake inaanzisha mnada huo utakaochangia mapato ya Manispaa.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini: Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.