Ni agizo lake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Omari Mgumba alipokuwa kwenye maadhimisho ya siku ya chakula duniani yenye kaulimbiu isemayo "Dunia bila njaa 2030 inawezekana", yaliyoadhimishwa kimkoa katika kituo cha kilimo Malolo, Kata ya Mabwepande, Manispaa ya Kinondoni.
Amesema maadhimisho haya yanayoadhimishwa tarehe 16/10 ya kila mwaka ni maadhimisho yenye lengo la kuonesha umuhimu wa kukabiliana na baa la njaa, kwani kauli mbiu ya mwaka huu inasadifu hayo na inatakiwa kutekelezwa kwa wakulima wetu kufanya kilimo cha uzalishaji unaozingatia mahitaji, upatikanaji na ubora wa bidhaa ili kukabiliana na changamoto ya Masoko.
"Tulime kwa kuzingatia mahitaji, ubora, na masoko, kwani ubora ndio utakaosababisha bidhaa zetu ziuzike kwa urahisi". Amesisitiza Naibu Waziri.
Aidha Naibu Waziri huyo pia amewataka wasindikaji wa vyakula kuanzisha chama kikuu cha ushirika kitakachowaweka pamoja na kuwawezesha kupata mikopo kutoka kwenye mabenki na kubadilishana uzoefu utakaowasaidia kuongeza tija katika uzalishaji.
Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, Mratibu wa wa maadhimisho hayo kwa Manispaa ya kinondoni ambaye pia ni Mkuu wa idara ya Kilimo Ndg Salehe Hija amesema kwa sasa kituo kinafanya utafiti wa ipi mbegu bora itakayoongeza tija katika Kilimo na kusaidia kupata mazao yanayohitajika hasa kwa wateja.
Maadhimisho hayo yaliyoadhimishwa kimkoa katika Kata ya Mabwepande Manispaa ya Kinondoni na kushirikisha wajasiriamali, wakulima na wasindikaji kutoka Halmashauri ya Ubungo, Ilala, Kigamboni na Temeke, pia yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali, kadhalika na wadau mbalimbali kama vile KOICA na NMB.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.