Wakandarasi wa barabara kote nchini wametakiwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, na kwa weledi mkubwa wakizingatia sheria, kanuni na taratibu katika kuhakikisha wanafikia viwango vya ujenzi vilivyokubaliwa pamoja na ubora uliokusudiwa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Alli Hapi alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea utekelezaji wa barabara zinazojengwa chini ya mradi wa DMDP, pamoja na zile zinazofanyiwa matengenezo chini ya TARURA.
Amesema Serikali imeamua kuelekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha inarejesha miundombinu iliyoharibika pamoja na kujenga miundombinu mipya inayoendana na ongezeko kubwa la watu, kwa kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora na viwango vinavyokubalika.
"Serikali inafanya kazi kubwa katika Wilaya ya Kinondoni kurejesha miundombinu ambayo iliharibika, iliyojengwa zamani, lakini pia kujenga miundombinu mipya, ambayo inaendana na idadi ya ongezeko la watu, na ongezeko la kiasi kikubwa cha maji kinachotokana na mvua katika misimu mbalimbali.......nitoe Rai kwa watu waliopewa dhamana ya kuhakikisha barabara, mitaro pamoja na miundombinu yote ambayo tumeitembelea inajengwa, wakiwemo wakandarasi na wahandisi, wafanye kazi kwa kuzingatia weledi, ubora na viwango vya hali ya juu, hatutamvumilia Mhandisi yeyote au Mkandarasi yoyote, atakayekwenda kutujengea barabara chini ya viwango"Amesisitiza Hapi
Naye Maneja wa TARURA Manispaa ya Kinondoni Bw. leopod Rungi amewaasa wananchi kutokufanya Maendeleo yeyote pembezoni mwa hifadhi ya barabara, kwani kwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na watakaobainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Katika hatua nyingine Mratibu wa DMDP Manispaa ya Kinondoni Bw. Mkelewe Tungaraza ameahidi kutekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya la kuhakikisha wanasimamia ubora wa kazi zinazoendelea za ujenzi wa barabara pamoja na kuwashughulikia wale wote waliojenga pembezoni mwa hifadhi ya barabara kinyume cha sheria kwa kuwapa Notisi ya siku Saba ya kuondoa majengo yao wenyewe.
Barabara alizozitembelea Mkuu huyo wa Wilaya katika ziara yake ni pamoja na barabara ya Mikumi, Idrissa, Chemchem, Tanesco soko la Samaki, Mazinde Viwandani ,Viongozi pamoja na Jengo la ofisi za DMDP.
imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.