Wakandarasi wa barabara kote nchini wametakiwa kuhakikisha wanasimamia misingi ya kazi zao kwa kuhakikisha wanajenga barabara kwa kuzingatia ubora na viwango vinavyokidhi matakwa na malengo yaliyokusudiwa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mh. Suleiman Jafo alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea ujenzi wa barabara zilizopo chini ya mradi wa DMDP unaotekelezwa Manispaa ya Kinondoni.
Amesema ujenzi wa barabara hizi umetumia gharama kubwa, hivyo wahandisi wahakikishe wanasimamia viwango katika ubora uliokusudiwa bila kufanya mjadala wa aina yeyote unaonesha kwenda kinyume au tofauti na makubaliano hayo.
"Mimi sitarajii katika barabara hizi baada ya mwaka mmoja, miaka miwili tunaanza kuziba viraka, barabara hizi tunatumia gharama kubwa Sana na hata ile mixture yake ni ya tofauti, kwa hiyo niwatake wakandarasi na hasa nyie ma injinia wetu hakikisheni ubora mnausimamia, hakuna ku-compromise katika swala zima la ubora wa barabara hizi "Amesisitiza Jafo.
Ameongeza kuwa lengo la mradi huu wa DMDP ni kuhakikisha linatatua changamoto kubwa za barabara walizokuwa wakizipata wananchi hasa zile zilizokuwa zikikumbwa na mafuriko kwa kukosekana kwa mitaro yenye ubora na inayokidhi viwango.
Kwa upande wake mratibu wa Mradi wa DMDP kinondoni Ndg Mkelewe Tungaraza ambaye pia ni Muhandisi wa barabara ameahidi kusimamia ujenzi huo kwa kuhakikisha viwango vya ubora uliokusudiwa vinafikiwa na kwa wakati.
Katika hatua nyingine Mh Jafo ameonesha kuridhishwa na hatua za ujenzi wa jengo uliofikiwa pamoja na ubora ulio nao jengo hilo linalotarajiwa kutumika kama ofisi na kuwataka wakandarasi hao kuhakikisha wanamaliza ujenzi huo kwa wakati na kuhakikisha linatumika kwa matumizi yaliyokubalika na si vinginevyo.
Waziri Jafo ametembelea barabara za DMDP za viwandani, M. M. K pamoja na kukagua hatua za utekelezaji wa jengo la mradi linalotarajiwa kutumika kama ofisi.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.