Wanandoa wametakiwa kuvumiliana katika maisha yao ya ndoa ili kuwaepusha watoto wao na janga la ukatili dhidi yao.
Wito huo umetolewa leo na Diwani wa Viti Maalum, Mheshimiwa Huba Issa, alipokuwa akihutubia mamia ya wanafunzi na wazazi wakati wa maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia na watoto Kata ya Msasani, Wilaya ya Kinondoni.
Mheshimiwa Huba, ambaye awali aliyapokea maandamano ya wanafunzi hao, alisema kuwa, " Ni vyema wazazi kuvumiliana katika maisha yenu ya ndoa ili kuepuka talaka ambazo hatimaye zinawafanya watoto kulelewa na wazazi wa kambo. " Alisema kuwa kutokana na malezi yasiyofaa ya baadhi ya wazazi wa kambo, huwapelekea watoto kufanyiwa ukatili hata na watu wa nje.
Alisema kuwa watoto wakipata malezi ya wazazi wote wawili huwajengea tabia njema katika maisha yao. Aidha aliwataka wanafunzi hao kujiepusha na ushawishi unaoweza kuwapelekea kufanyiwa ukatili.
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Msasani Bi. Husna Mnondo, alimweleza Mheshimiwa Huba kuwa Kata yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, wamefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya ukatili wa kijinsia haswa yaliyokuwa yakifanyika ufukwe wa Coco.
Awali Afisa wa Jeshi la Polisi Kata ya Msasani alisema kuwa hadi sasa kuna jumla ya kesi tano za vitendo vya ukatili wa kijinsia ambazo washatakiwa wa kesi hizo wamehukumiwa vifungo virefu magerezani.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini: Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.