Jumla ya vituo 292 vyatarajiwa kutoa huduma ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV vaccine) awamu ya kwanza kwa wasichana 5,562 wenye umri wa miaka 14, katika Manispaa ya Kinondoni.
Hayo yamethibitishwa leo na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mh Benjamin Sitta, alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa chanjo ya mlango wa kizazi uliofanyika katika kituo cha Afya Magomeni na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama na Serikali.
Amesema kwa idadi hii ya wasichana kupata chanjo ni mwanzo mzuri na pia kutasaidia kupunguza kiasi kikubwa cha ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huu.
"Kwa namna ya pekee, nimpongeze Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na uongozi wake mzima, kwa kukaa na kuumiza kichwa, na kuja na jambo jema kama hili, la kuwanusuru watoto wetu wa kike kwa chanjo hii ya saratani ya mlango wa kizazi, Mungu awabariki sana "Amesisitiza Meya.
Akitoa ufafanuzi wa chanjo hiyo kwa mgeni rasmi katika taarifa iliyosomwa kwake na Sr. Edith Mboga ambaye ni mratibu wa afya ya Mama na mtoto Kinondoni amesema, idadi hiyo inajumuisha wasichana 4,581 waliopo mashuleni na 892, waliopo katika jamii.
Ameongeza kuwa uzinduzi huu utawezesha huduma kuanza kutolewa kwa kushirikiana na wadau wote, wakiwemo wazazi, walezi, viongozi wa Serikali za mitaa, Kata Wilaya pamoja na viongozi wa dini.
Akitoa mchango wake Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dr. Festo Dugange amesema virusi hivi vya HPV huambukizwa kwa njia ya kujamiiana na ndio maana chanjo hii itahusisha wasichana wa umri wa miaka 14, kwani wanasadikiwa kutokuanza kwa mambo ya kujamiana.
Aidha amewaasa wanawake kuwa na utaratibu wa kupima afya zao kwani kwa kufanya hivyo kutaepusha madhara makubwa kutokea, hasa ikizingatia ugonjwa huu wa saratani ya shingo ya kizazi dalili zake huchelewa kujulikana.
Kinondoni imejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya Afya, wakiwemo waalimu wa shule za msingi na Sekondari, ikiwa ni mkakati wa pamoja kuhakikisha uelewa unatolewa kwa wazazi, na walezi ili kuhimiza wasichana wao kupata chanjo hii.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.