Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Songoro Mnyonge akifuatana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi Hanifa S. Hamza jana walipokelewa rasmi kwenye Makao Makuu ya Manispaa ya mji wa Loudi na kufanya mkutano na viongozi wa mji huo wakiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Meya anayeshughulikia utendaji(Executive Vice Mayor) Mheshimiwa Jiang Tianthai.
Viongozi wengine waandamizi waliohudhuria mazungumzo hayo ni Makamu wa Pili wa Meya, Mhe. Yu Min, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Tawala cha China cha CPC wa Manispaa ya Loudi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Manispaa ya Loudi, Mhe. Deng Wei, Mkurugenzi anayeshulikia elimu katika Manispaa ya Loudi, Mhe Liu Guoliang na Mkurugenzi wa Utamaduni, Michezo, Radio na Utalii wa Manispaa ya Loudi, Mhe Peng Yiling.
Akiongea katika mkutano huo, Makamu wa Kwanza wa Meya Mhe. Jiang aliyemwakilisha Meya wa Manispaa hiyo, Mhe. Zeng Chaoqum ambaye yupo safarini nje ya China alisema, Manispaa ya Loudi imejidhatiti kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni katika nyanja za maendeleo ya kijamii kama afya, elimu, michezo, miundombinu, udhibiti wa taka na masuala ya TEHAMA.
Alisema Madiwani na watendaji wa Kinondoni wanakaribishwa Loudi ili kwa pamoja waweze kubadilisha uzoefun a kutumia utaalam kwa faida ya wana Kinondoni na Tanzania kwa ujumla
Akiongea katika mkutano huo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe Songoro Mnyonge aliutaka uongozi wa mji wa Loudi kuisaidia Manispaa ya Kinondoni katika utaalam wa nyanja za elimu, uchumi, miundombinu,afya na michezo kwani wao wamepiga hatua kubwa katika maeneo hayo na mengineyo yabayoweza kuwa kichocheo cha maendeleo ya wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni,Bi Hanifa Suleiman Hamza aliwapongeza viongozi wa Loudi kwa mapokezi mazuri na kuwaomba waisaidie Kinondoni kufikia malengo ya kuwatumikia wananchi kwa maendeleo ya kasi zaidi.
Mapema asubuhi viongozi wa Manispaa ya Loudi waliwatembeza Meya, Mkurugenzi na Afisa Uwejezaji wa Manispaa, Bw. Shedrack Mbonika kwenye kiwanda cha kuzalisha vifaa vya michezo cha Inlang ambako walisaini makubaliano "MoU" ya kuisaidia timu ya Manispaa ya KMC FC vifaa vya michezo, walitembelea Shule ya Kati ya Xingxing ambayo inatumia teknolojia ya habari kufundisha wanafunzi
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.