VIKUNDI 115 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vimeaswa kutumia vizuri mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kukuza uchumi, kuongeza kipato na kutengeneza ajira.
Kauli hiyo imetolewa Februari 18, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo yenye jumla ya shilingi za Kitanzania 2,555,333,332.
Vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo ni vikundi 11 vya watu wenye ulemavu waliopata shilingi za Kitanzania 297,754,580; Wananwake vikundi 73 vilivyopata shilingi za Kitanzania 1,239,150,000 na Vijana vikundi 31 ambao wamepata shilingi za Kitanzania 1,018,428,742.
Mheshimiwa Mtambule alisema, "Manispaa imetekeleza jukumu lake la kisheria la kutoa mikopo isiyo na riba kwenu, hivyo ni jukumu lenu kuwajibika kutumia mikopo hii vizuri ili mpate faida, mkuze uchumi na kutengeneza ajira. Simamieni vizuri biashara zenu ili mrejeshe mikopo yenu na msimkatishe tamaa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Chama cha Mapinduzi na Manispaa yenu".
Aidha, aliwataka wanufaika hao kutoielekeza mikopo hiyo kwenye shughuli zisizo kusudiwa. Pia aliwataka wanufaika kufanya biashara katika mazingira salama na safi.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Mtambule ameipongeza Manispaa ya Kinondoni kwa kutoa mikopo inayotokana na asilimia kumi kwa utimilifu. "Kuna Halmashauri nyingi nchini hazifikii malengo ya utoaji mikopo hii kwa utimilifu, lakini Manispaa yetu imekuwa inaongoza kwa kutoa mikopo. Nawapongeza sana".
Akitoa taarifa ya utoaji mikopo hiyo tangu mwaka 2017/2018, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Hanifa Suleiman Hamza, alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa mikopo hiyo ni ya kipindi cha robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwamba, "Halmashauri itaendelea kuiwezesha jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli kujiletea maendeleo ili kufikia azma ya jamii kujikwamua kiuchumi na kupiga vita umasikini."
Alieleza kuwa Halmashauri inaendelea na jitihada za kuhamasisha jamii kuunda vikundi na kuvisajili ili kuweza kupata mikopo isiyo na riba kupitia fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani pamoja na pesa inayotokana na marejesho.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.