Manispaa ya Kinondoni kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii leo tarehe 20 Juni, 2022 imeendesha mafunzo ya siku moja kwa wanufaika wa mikopo ya asilimia kumi inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia vema na kurejesha mikopo ambayo Manispaa ya Kinondoni kila mwaka huitoa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akifungua mafunzo hayo Mheshimiwa Anna Lukindo, Diwani wa Kata ya Mbezi Juu amevitaka vikundi vyote 286 kuwa waaminifu katika kufanya marejesho pindi wanapotakiwa kuanza kufanya marejesho ili waweze kukopesheka tena na kuwapa nafasi wengine wanaotaka kukopa.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Kinondoni, John Deogratius amesema kuwa mikopo inayotolewa ina lengo la kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi hivyo ni vyema wakatumia fursa ya kuchukua mikopo na kuitumia kikamilifu ili waweze kufanya marejesho kwa wakati.
Wanufaika wa mikopo pia wamepata fursa ya kufundishwa na kuelekezwa jinsi ya kutumia mikopo hiyo kama ilivyokusudiwa na kujua namna ya kutafuta masoko katika biashara zao, uandaaji wa mipango ya biashara, uwekaji wa kumbukumbu pamoja na kufahamu namna ya uwekaji wa akiba.
Aidha, mikopo hiyo ya asilimia kumi (10%) ya fedha zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri imetolewa kwa vikundi vya wanawake 182, vijana 90 na watu wenye ulemavu 14 kwa lengo la kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali zitakazowawezesha kujiongezea kipato na kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi na kupiga vita umasikini.
Imeandaliwa na:
Kitengo cha Habari na Uhusiano,
Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.