Vijana kote nchini wametakiwa kuhakikisha wanajenga Utamaduni wa kujishughulisha na shughuli za kujikwamua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kujiunga kwenye vikundi endelevu vya vicoba ili waweze kupata elimu ya ujasiriamali kwa lengo la kukabiliana na changamoto za ajira.
Agizo hilo limetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Ali Hapi alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa taasisi ya BUTA Vicoba endelevu iliyofanyika katika Kata ya Bunju Manispaa ya Kinondoni.
Amesema vijana wengi wamekosa Utamaduni wa kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali kitu ambacho hakimjengi katika kujikwamua kiuchumi, kimaendeleo na kifikra kuelekea uchumi wa viwanda.
"Wasichana hawana Utamaduni wa kuweka akiba, wengi wadada zetu wanawekeza kwenye urembo, wakishafika umri wa kuwa wamama ndio wanaanza kuchangamkia fursa za uchumi Kama hizi, kwa hiyo kinamama popote mlipo wahamasisheni mabinti zenu na kinababa wahamasisheni mabinti zenu wakiwa bado wanaumri mdogo wawe na Utamaduni wa kuweka akiba, wawe na Utamaduni wa kushiriki kwenye shughuli za ujasiriamali" amesema Hapi
Amesema Serikali inahitaji sekta binafsi pamoja na wajasiriamali ili kwa pamoja tuweze kuwafikia watu wengi zaidi ili waweze kujikwamua na tatizo la ajira.
"Ndugu zangu ninyi mnafahamu ya kwamba Serikali inayomajukumu makubwa ya kufanya katika kujenga uchumi wa wananchi wetu, lakini Serikali peke yake haiwezi kufanya jukumu hilo, tunawahitaji sekta binafsi tunahitaji wajasiriamali, tukishirikiana kwa pamoja unauwezo wa kuwasaidia na kuwafikia wananchi wengi zaidi, tunafahamu tunalo tatizo la ajira, tunao vijana, tunao kinamama ambao hawana ajira, lakini nataka kuwakikishia kwamba hakuna serikali duniani ambayo inauwezo wa kumaliza tatizo la ajira kwa asilimia miamoja haipo " amefahamisha Hapi
Aidha amefurahishwa na wanachama hawa wa vicoba endelevu kushirikiana na taasisi za kifedha kama mabenki na mashirika mbalimbali, kadhalika kuwa na utaratibu wa kujiunga kwenye mifuko ya hifadhi ya kijamii inayowawezesha wanachama kupata matibabu,mikopo na mafao ya uzeeni.
Naye Rais wa vicoba endelevu Tanzania Bi Devota likokola ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuruhusu siku ya kuondoa umaskini duniani kuwa siku ya Vicoba.
Amesema kwa mujibu wa taarifa ya baraza la vicoba Tanzania mpaka sasa vimefikia zaidi ya vicoba endelevu laki moja, vyenye wanachama zaidi ya milioni mbili na laki mbili na vyenye mzunguko wa fedha uliofikia kiasi cha trilioni moja na milioni miambili .
Katika hatua nyingine Mh Hapi amewataka wanachama hao wa vicoba endelevu kupanua wigo mkubwa ili waweze kuwafikia wajasiriamali, waalimu, wafanyakazi wa Serikali, wafanyabiashara wa kwenye masoko, ili kwa pamoja tuweze kusaidiana kulikwamua gurudumu la maendeleo.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.