Vigezo 14 vilivyotumika katika mkakati wa Serikali wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi yenye kuchochea Mapato, vyaipatia Kinondoni jumla ya tsh bil 9, kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa Magomeni.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mh. Suleiman Jafo, katika hafla ya uzinduzi wa uwekaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika mamlaka za Serikali za Mitaa iliyofanyika katika ukumbi wa Treasure square Mkoani Dodoma.
Amesema mingoni mwa Halmashauri 17, kati ya 185, zilizoshindanishwa, Kinondoni imeibuka kidedea na kufikia vigezo vya kupatiwa fedha hizo, na kuwataka Mkurugenzi wake Ndg Aron Kagurumjuli, pamoja na Meya wake Mh Benjamin Sitta kuhakikisha wanasimamia fedha hizo kwa lengo lililokusudiwa.
Akiainisha vigezo hivyo vilivyotumika, Mh Jafo amesema lengo ni kuziwezesha mamlaka za Serikali za Mitaa, kujisimamia wenyewe Katika kutekeleza mpango mkakati wa miradi hiyo itakayoongeza Pato la Halmashauri.
Amevitaja vigezo hivyo kuwa ni andiko la mradi, upembuzi yakinifu, mtiririko wa fedha, uwezo wa kuongeza mapato, uwezo wa Halmashauri kusimamia mradi, uthibitisho wa umiliki wa ardhi, pamoja na uchambuzi wa viashiria vya uhimilivu.
Nyingine ni uwezo na mpango wa Halmashauri kujitegemea, michoro na usanifu, mpango wa matumizi ya eneo la mradi, hati safi ya ukaguzi wa hesabu, mpango mkakati wa Halmashauri, nyaraka za mradi na vielelezo kuchambuliwa na sekretarieti ya Mkoa husika, pamoja na uchambuzi ulioidhinishwa na OR-TAMISEMI.
Hafla hiyo ya utiaji saini imehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dr. A. Kijaji, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya, Wah. Wabunge, pamoja na Wakuu wa Mikoa.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.