Wananchi wa Kata ya Ndugumbi, Manispaa ya Kinondoni, wameaswa kuwa mabalozi wa usafi katika maeneo wanayoishi ili kuepukana na mlipuko wa magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira.
Wito huo ulitolewa Machi 11, 2024 na Afisa Usafishaji wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Shedrack Maximilian, kwenye kampeni ya "Mguu Kwa Mguu Kitaa" ambayo imelenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazoikumba sekta ya usafi, watoa huduma za usafi wa mazingira na wapokeaji huduma za usafi katika Kata za Wilaya ya Kinondoni.
Akiwa kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na Maafisa kutoka Wilaya ya Kinondoni, Viongozi kutoka Kata na Mitaa pamoja na Wananchi wa Mitaa mbalimbali kutoka Kata ya Ndugumbi Bw. Maximillian aliwaasa Wananchi hao kuwajibika ipasavyo kufanya usafi kila siku badala ya kusubiri usafi wa mwisho wa mwezi ili kuepukana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
"Sisi Wananchi tunao wajibu wa kulinda afya zetu kwa kusafisha mazingira yetu na pia hakikisheni mnaishi kwenye Nyumba zenye huduma za vyoo ili kuepuka mlipuko waa kipindupindu." alisema Bw. Shedrack.
Katika kampeni hiyo Wananchi walionywa kutotupa taka hovyona pia wamekumbushwa wajibu wao kwenye kutunza usafi wa mazingira, ikiwemo kuhakikisha taka wanazozalisha wanahifadhi ili zichukuliwe na magari ya taka.
Katika kusisitiza hilo Bw.Maximilian alisema "Kuna haki na wajibu ili kupata haki inabidi mtu atimize wajibu wake, ni wajibu wenu kufanya usafi".
Pia, Wafanyabiashara waliaswa kuzingatia usafi katika maeneo yao ya biashara ili kulinda afya za wateja na Wananchi wanaoishi maeneo jirani.
Kampeni ya "Mguu Kwa Mguu Kitaa" imelenga kupita katika maeneo yote ndani ya Manispaa ya Kinondoni ili kusikiliza kero zinazoikumba sekta ya usafi kutoka pande zote mbili za watoa huduma na wahudumiwa.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.