Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ameuhakikishia Umma wa wakazi wa Kinondoni kuwa suala la ULINZI na USALAMA wa raia ni la kipaumbele.
"Naomba niwatoe hofu wakazi wote wa Kinondoni kuwa suala la ulinzi ni kipaumbele changu. Natoa wito kwa vijana wote wanaojiita panya road, ukanda huu hakuna utakapojificha tusikukamate. Ukanda huu si salama kwenu." DC Saad Mtambule alisema.
Aidha amewataka wananchi kuhakikisha wanasaidiana na Jeshi la Polisi ili maeneo yote yanakuwa salama. "Polisi endeleeni kuimarisha ulinzi, hakuna kulala wala kupumzika ili maeneo yetu yawe salama."
"Wazazi na walezi hakikisheni mnatoa malezi mazuri kwa watoto. Aidha natoa onyo kwa wananchi wanaotoa taarifa za uongo zenye kuleta taharuki, hatua zitachukuliwa dhidi yao. Toeni taarifa sahihi na sisi tutakuja hapo haraka iwezekanavyo ili kuokoa maisha ya watu."
Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Bunju 'A' kufuatia taarifa za uzushi za uwepo wa vijana wahalifu maarufu kama panya road.
Kwa upande wao Wakuu wa Polisi Kawe na Mapwebande wamesema kuwa Jeshi la Polisi lipo tayari kukabiliana na jambo lolote la uhalifu litakalo jitokeza. Aidha, wamewataka wazazi na walezi kusaidiana na Jeshi hilo kuwafichua vijana wahalifu ili kuwadhibiti mapema.
Nao Wenyeviti wa Mitaa ya Kata za Mbweni, Bunju na Wazo Wilaya ya Kinondoni wamemuelezea Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Saad Mtambule kuwa hakuna tukio wala tishio la panya road lililojitokeza katika maeneo yao. "Tunakuhakikishia kuwa maeneo yetu kwa siku ya jana yalikuwa salama kabisa," alisema Bw. Zimwi ambaye ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mitaa Wilaya ya Kinondoni.
Imeandaliwa na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini: Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.