Wananchi wa mitaa ya Kisiwani, Mchangani na Sindano katika Kata ya Makumbusho, wameridhia kuachia baadhi ya maeneo katika makazi yao ili kupisha ujenzi wa barabara.
Mradi huo wa barabara yenye urefu wa kilomita 1.3 unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, unaunganisha barabara ya Ndugumbi hadi Mwinyijuma.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Mstahiki Meya Manispaa ya Kinondoni, Mheshimiwa Songoro Mnyonge, na Diwani wa Kata ya Makumbusho Mheshimiwa Mohammed A. Mohammed.
Ujenzi wa barabara hiyo unaosimamiwa na mradi wa DMDP utakuwa na upana wa mita 10. Aidha, mradi huo utahusisha uwekaji wa taa za barabarani na njia za waenda kwa miguu.
"Tumekuja kuwaomba wananchi mkubali kuupokea mradi huu. Muachie baadhi ya maeneo yaliyozidi na kuwekewa alama ili mradi uanze, alisema Mheshimiwa Mohammed.
Kufuatia majadiliano hayo, wakazi hao kwa kauli moja waliridhia mradi huo. Mzee Mashaka Kino, alisema kuwa, "tangu mwaka 1971 tumekuwa tukiomba kupatiwa barabara hii, nawaomba wananchi wenzangu tuukubali."
Kwa upande wake, Meya Songoro aliwashukuru wakazi hao na kuelekeza ujenzi wa mradi huo uanze mara moja. "Mradi huu unafaida nyingi, zikiwemo nyumba zenu kupanda thamani, usalama, biashara kufanyika mchana na usiku na hata huduma ya daladala itapatikana."
Imeandaliwa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.