Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla leo tarehe 30 Juni, 2022 amezindua kiwanda cha kuchakata taka na kuzigeuza kuwa mbolea mboji katika Kata ya Mabwepande, Manispaa ya Kinondoni kilichojengwa kwa gharama ya shilingi za Kitanzania bilioni 6 ikiwa ni ufadhili wa Serikali ya Ujerumani na Tanzania kupitia ushirikiano baina ya Jiji la Dar es Salaam na Jiji la Hamburg.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, RC Makalla amesema kiwanda hicho kimekuja wakati muafaka ambao bei ya mbolea imepanda kutokana na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine na kutoa wito kwa wananchi kununua mbolea hiyo.
Kiwanda cha uchakataji taka kinatarajiwa kutengeneza tani hamsini mpaka mia moja za mbolea ya mboji kwa siku ambayo itakayotumika kuongeza ukuaji mzuri wa mimea na kurudisha rutuba kwenye udongo uliokosa virutubishi na kuharibika.
Faida zitakazopatikana na mboji inayotengenezwa na kiwanda hicho ni pamoja na kusaidia mimea kukua vizuri wakati wa ukame, kusaidia mzunguko wa hewa kwenye udongo, kupunguza uchafu unaotupwa kwenye madampo pamoja na kuzuia uchafuzi wa mazingira.
Aidha RC Makalla amesema uwezo wa mkoa huo ni kuzalisha zaidi ya tani 23 za taka kwa siku hivyo kupatikana kwa kiwanda hicho kitasaidia kuwa na uhakika wa mahala pa kuzipeleka.
RC Makalla ametoa wito kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kusimamia vizuri uendeshaji wa kiwanda kwa kuhakikisha uzalishaji wa malighafi unakuwa wa kutosha.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.