Manispaa ya Kinondoni ina ziada ya vyumba vya madarasa 27 kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi 14,825 ambao wamefaulu mtihani wa kuingia kidato cha kwanza kwa mwaka 2022.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Hanifa Suleiman Hamza, amebainisha hayo wakati akitoa taarifa fupi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Amos Makala, ya ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa katika shule ya sekondari, Boko Mtambani.
Alisema ujenzi wa madarasa hayo unaendelea vizuri na upo katika hatua za mwisho. Alisema, "Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, sisi tulijiongeza kidogo, tuna ziada ya vyumba vya madarasa 27 ambavyo vitawapokea wanafunzi wetu waliofaulu".
Aliongeza kuwa, Manispaa ya Kinondoni imeongoza katika matokeo hayo kimkoa kwa kupata asilimia 98.5 ya ufaulu na hivyo kushika nafasi ya kwanza.
Naye Mheshimiwa Makala, ameupongeza uongozi wa Manispaa ya Kinondoni kwa hatua nzuri ya ujenzi na kusisitiza ujenzi huo umalizike mapema". Nawapongeza, mpo kwenye hatua nzuri na hongereni kwa kuongeza fedha zenu katika ujenzi wa madarasa mengine".
Aidha ameshauri kujengwa uzio wa shule hiyo mara baada ya ujenzi wa madarasa kukamilika ili kuyaweka mazingira ya shule hiyo katika hali ya usalama.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mheshimiwa Songoro Mnyonge, licha ya kupongeza juhudi hizo na kuahidi ujenzi wa uzio wa shule hiyo, pia aliahidi kukamilishwa kwa ujenzi wa uwanja wa mpira uliopo Mwenge ndani ya wakati ifikapo Machi, 2023.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini: Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.