Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mheshimiwa Songoro Mnyonge asisitiza matumizi ya nishati safi ili kuokoa uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko makubwa ya tabia nchi.
Mheshimiwa Songoro aliyasema hayo Aprili 20, 2024 katika uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira na matumizi ya nishati safi uliofanyika katika Kata ya Mikocheni Mtaa wa Michungwani, Manispaa ya Kinondoni.
Alisema, "Katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha, niwaombe wakazi wa Mikocheni na viunga vyake vyote kutunza mazingira.
Hili ni jukumu letu. Tufanye usafi na kutumia nishati safi ya gesi."
Aidha, Mheshimiwa Songoro amempongeza Mheshimiwa Rehema Mandingo, ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu, kwa kuanzisha kampeni hiyo ikihamasisha pia matumizi ya nishati safi. Kampeni hiyo, itasaidia Kata ya Mikocheni na Wilaya ya Kinondoni kwa ujumla kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wake Mheshimiwa Mandingo aliwashukuru Wanawake wa Kata ya Mikocheni kwa kujitokeza katika kuunga mkono kampeni hiyo yenye kauli mbiu "Wanawake na Mazingira."
Kadhalika, Mheshimiwa Mandingo aliiomba jamii ya Mikocheni kuwa walezi wazuri na kufuatilia mwenendo mzima wa watoto wao ili tuweze kutokomeza masuala yote ya ukatili wa watoto wote ndani ya Kata hii na Wilaya nzima ya Kinondoni.
Katika uzinduzi huo Mheshimiwa Mandingo alitoa mitungi ya gesi 20 yenye uzito wa Kilogramu 14.8 kwa Wanawake wajasiriamali wa Kata ya Mikocheni kwa lengo la kuokoa matumizi ya kuni na mkaa.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.