Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wametakiwa kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 itolewayo na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa usahihi ili kubadilisha maisha yao.
Hayo yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge leo Julai 10, 2023 alipotembelea banda la Manispaa ya Kinondoni katika maonyesho ya 47 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Saba Saba).
“Leo nimepata fursa ya kutembelea banda letu la Manispaa ya Kinondoni ikiwa ni washiriki wa maonyesho ya 47 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Saba Saba) ambapo tumeweza kutoa fursa kwa wajasiriamali mbalimbali ambao ni wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 kwa akina mama, vijana na watu wenye ulemavu hivyo niwaombe wananchi wote wa Manispaa ya Kinondoni kuchangamkia fursa hiyo", amesema Mhe. Songoro.
Mhe. Songoro amesema mikopo hiyo imekuwa na faida kubwa kwa wakazi wa Manispaa ya Kinondoni kwani imeweza kubadilisha maisha ya vikundi mbalimbali vya wajasilimali waliopata mikopo hiyo.
Aidha, Mstahiki Meya Songoro ametumia fursa hiyo kuwaomba wanufaika wa mikopo hiyo kurudisha mikopo hiyo kwa wakati ili iweze kutumika na kuwanufaisha watu wengine wenye uhitaji.
Nae Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kutoka Manispaa ya Kinondoni Bi. Magreth Jackson amewaomba wanufaika wa mikopo ya Halmashauri kubuni miradi yenye tija na inayoweza kutoa ajira kwa wengine.
“Niwasisitize wanufaika wa mikopo hii kuangalia miradi yenye tija na inayotoa ajira kwa wengine ili tuweze kufikia lengo la mikopo hii na kuwawezesha kurudisha mikopo hiyo kwa wakati", amesema Bi. Magreth.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini: Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.