Zaidi wa Wageni 2,000 kutoka mataifa mbalimbali Afrika watahudhuria Mkutano wa Kimataifa kuanzia Julai 25 hadi 26, 2023.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mheshimiwa Saad Mtambule wakati akiongea na Wajumbe wa Kamati ya Lishe, Wilaya ya Kinondoni.
Ameongea hayo alipokutana na Wenyeviti wa Mtaa, Watendaji wa Mtaa, Watendaji wa Kata, Madiwani na Watendaji wa Ofisi ya Mkurugenzi wakati wa kutoa taarifa ya ugeni mkubwa wa wageni hao ikiwa ni mwaliko na heshima kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa wa Afrika unaozungumzia maendeleo ya rasilimali watu.
Mpaka sasa nchi 25 zimethibitisha kushiriki mkutano huo utakaojadili namna ambavyo rasilimali watu za Afrika zilivyo hivi sasa kielimu, kiafya na kidemokrasia.
"Tunatarajia ugeni mkubwa sana, utakaojadili Maendeleo ya Raslimali watu katika Bara la Afrika," alisema na kuongeza", hivyo niwaombe sana tuendelee kuimarisha Ulinzi na Usafi katika maeneo yetu".
Alisema kuwa wageni hao ambao wengi watafikia katika maeneo ya Wilaya ya Kinondoni, "tunatakiwa tuimarishe ulinzi ili pasiwepo na hitilafu wakati wa wa ugeni huo".
Aidha, aliwaomba Watendaji hao, kushiriki pia katika Mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM Taifa ambao utafanyika Viwanja vya Tanganyika Packers Julai 29 na kuongeza kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye mkutano huo.
Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Mtambule amewahimiza Watendaji wa Kata kuhakikisha wanasimamia masuala ya lishe katika maeneo yao haswa kwa makundi maalum. "Tukisimamia lishe vizuri tutazalisha Raslimali watu iliyo bora. Tuhakikishe tunafikia malengo ya vigezo tulivyowekewa katika kusimamia lishe katika Kata zetu".
Kikao hicho kimekutana kikiwa ni kujadili taarifa ya tathmini ya utekelezaji Mkataba wa Lishe wa Robo ya Nne (Aprili-Juni).
Tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe katika Manispaa ya Kinondoni imeonekana kufanikiwa katika kipindi cha mwaka 2022/2023.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.