Wananchi wameaswa kuwa mabalozi wa kutoa taarifa na elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia unaofanyika kwa watoto. Mei 3, 2024, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti Ukimwi ya Manispaa ya Kinondoni, Mheshimiwa Joseph Rwegasira, alitoa wito huo wakati wa ziara ya Robo Tatu ya Mwaka ya Kamati hiyo iliyofanyika katika kituo cha Mkono kwa Mkono (One Stop Centre). Kituo hicho hutoa huduma za manusura kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia kilichopo katika Hopitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala.
Mheshimiwa Rwegasira alisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana na mamlaka husika katika kutoa taarifa kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika. Alisema kuwa kutoa taarifa ni jukumu la kila mwananchi na ni njia muhimu ya kuwalinda na kudumisha haki za watoto.
"Ukatili wa jinsia ni chanzo cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kutoa elimu kuhusiana na ukatili wa kijinsia na athari zake katika jamii. Tupeleke elimu hii bila kuchoka kwani elimu yako utakayopeleka kwenye jamii inaweza kuokoa watoto elfu moja," alisema.
Aidha Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Bi.Halili Halifa Katani, aliwaasa Wananchi kutoa taarifa zinazohusiana na ukatili wa kijinsia ndani ya Saa Sabini na Mbili ili kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa Watoto waliofanyiwa ukatili.
Alisema, "Wananchi wasisite kuwaleta watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili kwa wakati ili tuweze kuwaunganisha huduma mbalimbali ikiwemo kuwapatia Dawa za kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (PEP) pamoja na huduma ya ushauri nasaha."
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.