Ni agizo lake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Daniel Chongolo, alipokuwa akitoa maelekezo, katika kikao kazi cha Kamati ya Afya ya Msingi ya Wilaya, kilichofanyika leo kwa lengo la kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za Afya, ikiwemo utekelezaji wa kampeni ya ugawaji dawa kinga na tiba kwa magonjwa ya kichocho na Minyoo ya tumbo kwa wanafunzi wa shule za awali na msingi.
Amesema mada zinazoishi kuhusiana na masuala ya magonjwa ya jumla yanayoweza kuzuilika, ni kitu ambacho mwananchi anatakiwa kukumbushwa mara kwa mara kupitia watendaji ngazi ya Kata na Mitaa kwani asilimia kubwa yanatokana na uchafu na mazalia ya mbu.
"Nitoe Rai idara ya Afya, tusisubiri dharura kwenye kushughulikia magonjwa ya mlipuko, katika vikao vyenu, ngazi za Kata,Mikutano ya wananchi, tengenezeni mpango wa uwasilishaji mada zinazoishi, mada inayoishi katika magonjwa ya jumla kama kipindupindu, kichocho, kwani haya msingi wake ni uchafu" Amebainisha Mh.Chongolo.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dr. Festo Dugange amesema, Manispaa ya Kinondoni inavyo vituo 187, vya kutolea huduma za Afya vikihusisha hospitali, zahanati, kliniki, na martenity home ambavyo, kati yake 27 ni vya Serikali, na 160, ni vya binafsi, taasisi za Serikali, na Mashirika ya kidini tunavyoshirikiana navyo katika kuboresha utoaji huduma za Afya, ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zinazojitokeza, na kuweka mikakati ya maboresho katika sekta hiyo.
Akitoa taarifa ya kampeni ya ugawaji wa dawa kinga na tiba kwa magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo kwa wanafunzi wa shule za awali na Msingi, mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Dr. Neema Mlole amesema, Kinondoni imelenga kufikia wanafunzi 121,086 , wenye umri kuanzia miaka 5 hadi 14, walioandikishwa katika shule za awali na Msingi, 157, zilizopo ndani ya Kata 20 za Manispaa ya Kinondoni.
Ameongeza kuwa, katika kampeni hii, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya maendeleo ya jamii, jinsia ,wazee na watoto kupitia kitengo cha Mpango wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele imeshachukua hatua stahiki kuelekea kwenye utekelezaji ikiwemo kutoa elimu kwa wazazi na walezi, kutoa elimu kwa wagawa kinga tiba hizo watakaoshiriki zoezi, kusambaza dawa na vifaa maalumu, pamoj na mpango wa kuandaa chakula kwa wanafunzi kabla ya kuwapa kinga tiba hizo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya, kwenye kikao hicho kilichohusisha Kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya, wawakilishi wa mashirika ya dini, pamoja na wajumbe wa kamati, ameitaka idara ya Afya kuhakikisha inashughulikia maduka ya dawa muhimu, pamoja na hospitali bubu zinazoendeshwa bila vibali wala utaratibu, ili kujiepusha na madhara ya kiafya yanayoweza kutokea kwa watumiaji.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.