Katika kujiandaa kukabiliana na mvua za Vuli zinazoweza kusababisha El Nino, Manispaa ya Kinondoni imetakiwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika ngazi zote ili kuepukana na maafa.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mheshimiwa Saad Mtambule, katika kikao cha majadiliano namna ya kukabiliana na changamoto za mvua hizo, alisema “Viongozi na wananchi shirikianeni katika kuboresha miundombinu, na mikakati kuzuia maafa tarajiwa.”
Hadi sasa, Mitaa 40 kati ya 106 na Kata 16 kati ya 20 zimebainika kuwa hatarini kupata mafuriko. Kata hizo ni Bunju, Kigogo, Magomeni, Mzimuni, Hananasif, Tandale, Kawe na Kijitonyama. Kata nyingine ni Mbweni, Mbezi Juu, Mwananyamala, Makumbusho, Kunduchi, Kinondoni, Mikocheni na Msasani.
Ikiwa ni maandalizi ya kujiandaa na kukabiliana na El Nino, pamoja na mambo mengine, Manispaa inaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya El Nino huku ikihamasisha watu wanaoishi maeneo hatarishi kuhama.
Hatua nyingine ni kuendelea kuimarisha barabara, madaraja na kusafisha mifereji na mito mikubwa na midogo ambapo hadi sasa mto Ng’ombe umesafishwa.
Kwa mujibu wa Mratibu na Msimamizi wa Maafa, Bw. Bakari Mlanzi, “Kinondoni imejipanga ipasavyo kukabiliana na maafa ya mvua za El Nino.”
Anaendelea kueleza kuwa, “tunaendelea kuhuisha Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa Wilaya; tunandaa Mpango wa Dharura wa Kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El Nino, kuainisha raslimali zinazoweza kutumiwa katika kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El Nino, ikiwepo kuimarisha uwezo wa kutoa huduma za matibabu kwa waathirika, kutambua wadau wa misaada ya kibinadamu, kutambua wadau wakushiriki katika juhudi zinazoendelea za kujiandaa, kupambana na kurejesha hali.”
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.