NI KUFUATIA ZIARA YA DC -HAPI KATIKA KATA 20, ZA WILAYA YAKE, AKISIKILIZA, AKIKAGUA AKIJIRIDHISHA, AKISHAURI NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI WAKE KWENYE MKUTANO WA HADHARA.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Ali Hapi amezindua operesheni ya siku 36, ya kusikiliza, kushauri na kutatua kero za wananchi katika Wilaya yake, ikiwa ni njia mojawapo ya kujiridhisha na utekelezaji wa utoaji huduma sahihi kwa wananchi wake, kadhalika na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi unaozingatia sera, haki, wajibu, viwango na usawa katika upatikanaji wa huduma hizo.
Operesheni hiyo imezinduliwa leo alipokuwa katika ziara yake hiyo na baadae kuzungumnza na wananchi wa Kata ya Tandale katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanjani hapo ambapo wakuu wa idara na vitengo, pamoja na taasisi mbalimbli zilitakiwa kutoa majibu ya kero hizo kwa wananchi.
Amesema azma yake kama Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, pamoja na Serikali inayotuongoza ni kuona, kuhakikisha na kujiridhisha na huduma zitolewazo kwa wananchi katika nyanja zote kwani ndio msingi imara uletao matokeo chanya katika kusukuma gurudumu la Maendeleo linaloenda sambasamba na uchumi wa viwanda kwa nchi yetu.
"Ni lazima sisi kama viongozi, tunaolipwa mishara kutokana na kodi zenu wananchi, tuhakikishe kazi zinafanyika, tujiridhishe wananchi wanasikilizwa, wanapatiwa huduma stahiki, na kero zinatatuliwa, watumikieni wananchi kwa wema, kwa upendo, kwa utii na kwa haki hiyo ndiyo ari ya Serikali ya awamu ya tano ya HAPA KAZI TU" Amesisitiza Hapi.
Alipokuwa akifafanua dhumuni hilo la operesheni yake amesema ziara hiyo itakuwa ni ya siku 36, ambapo kwa siku 20, atakuwa kila kata kukagua miradi, kusikiliza na kutatua kero, na kwa siku 16, ni kwa wakuu wa idara na vitengo wa Manispaa hiyo kuweka kambi katika Kanda 4 atakazozipanga kwa lengo la kuhakikisha kero, na maelekezo yanafanyiwa kazi.
Alipokuwa akifafanua utekelezaji wa ilani ya CCM, kwa Wilaya yake, Mkuu huyo amesema, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Wilaya yake ilitenga bilioni 3.8,kwa ajili ya mikopo ya wanawake na vijana, ambapo hadi sasa zimetumika tsh bilion 1.9, ambayo ni sawa na asilimia 50%, imesikiliza kero za ardhi zisizopungua 637, pamoja na kutengeneza madawati yasiyopungua 7 , 319.ili kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa huduma bora za elimu.
Kadhalika akijibu kero za ardhi zinazoshughulikiwa na mabaraza ya Kata Hapi alifafanua kuwa mabaraza ya Kata, hayapaswi kisheria kusikiliza shauri linalozidi thamani ya tsh milioni tatu, na kwa upande wa kero ihusuyo upungufu wa madawa kwenye zahanati na vituo vya Afya amemtaka Mganga Mkuu wa Manispaa ndg Festo Dugange kutoa elimu kwa wananchi ya zipi dawa zinapatikana katika vituo vya Afya na Zahanati hizo
Hii ni safari ya mafanikio kuelekea siku 26, za kuwatumikia wananchi kwa ukaribu zaidi, ambapo ameanzia katika Kata ya Tandale na baadae kuongea na wanachi kwenye mkutano wa hadhara ambapo kero mbalimbali zihusuzo afya, mazingira, miundombinu, maswala ya vyeti vya kuzaliwa,maswala ya elimu zimetatuliwa.
Imeandaliwa na
Ofisi ya Uhusiano na habari.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.