NI KWA KURASIMISHA EKARI 366 ZA ARDHI ENEO LA BOKO DOVYA, MANISPAA YA KINONDONI.
Serikali kupitia Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi, Mh Willium Lukuvi imemaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati yake na wananchi, kwa kurasimisha eneo hilo lenye ekari 366 lililokuwa linatumiwa kwa makazi na wavamizi tangu kutwaliwa kwake.
Akiongea na wakazi wa Boko Dovya katika mkutano na wananchi hao, Mh Lukuvi amesema, eneo hilo lililokuwa linamilikiwa na familia ya Somji lilitwaliwa na Serikali kwa manufaa ya umma na kabla ya kuendelezwa kwake wananchi wakavamia na kufanya makazi kinyume cha Sheria.
Amesema maeneo ya ardhi yanapotwaliwa na Serikali ni kwa manufaa ya Umma na ni lazima yaheshimiwe na si vinginevyo, hasa ikizingatiwa nia ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dr. John Pombe Magufuli ni ya dhati kabisa ya kuona wananchi wake wanaondokana na migogoro ya ardhi isiyo yalazima.
Aidha ameongeza kuwa kwa urasimishaji huo kukamilika, wananchi wakazi wa eneo hilo yawapasa kuchangia gharama za uandaaji wa michoro ya Upimaji, pamoja na upatikanaji wa hati , ili waweze kupata hati zitakazowatambulisha uhalali wa umiliki wao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Alli Hapi, amemshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wake huo, na kuwatahadharisha matapeli watakaojitokeza kujipatia maeneo katika eneo hilo, au kuhamisha wenyeji kuwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani.
Kadhalika amepiga marufuku uuzaji, na ununuaji wa ardhi kiholela, au kufanya maendelezo yoyote katika eneo hilo mpaka pale zoezi la urasimishaji litakapokamilika.
Wakizungumnza kwa nyakati tofauti wananchi wakazi wa eneo hilo wamemshukuru Mh Magufuli kwa uamuzi huo, wa kurasimisha eneo hilo na kuahidi ushirikiano mkubwa katika zoezi zima la urasimishaji.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.