Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na maswala ya usalama wa mtoto liitwalo Save the Children kwa kushirikiana na PDF, leo limeendesha semina yenye lengo la kutoa elimu ihusuyo uandaaji wa bajeti na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2019/2020, kwa maswala mbalimbali ya watoto.
Akiendesha semina hiyo mwakilishi kutoka shirika la Save the children Bi Neema Bwaira amesema maswala yahusuyo watoto katika vitengo na idara ni mtambuka, na hivyo hatuna budi kuweka bajeti inayomgusa mtoto katika utekelezaji wa majukumu ya kilasiku.
Bi Neema pia ameainisha sifa ya bajeti ambayo ni rafiki kwa mtoto kuwa ni ile inayotekeleza sera za kiuchumi na za jamii ambazo ni rafiki na zinamaslahi mapana kwa watoto na inaangalia mahitaji muhimu ya watoto waishio katika mazingira magumu.
Ameendelea kuziainisha kuwa ni ile inayogusa sekta muhimu kama vile elimu, afya, maji safi, usafi wa mazingira, ni ile inayotoa fursa sawa za maendeleo na kuheshimu haki za watoto bila kujali makabila, dini, mikoa au rangi, na yenye kutengeneza mfumo bora na wezeshi katika mtiririko wa rasilimali unaomfikia mtoto kwa wakati.
Akianisha mpango wa bajeti na mchakato wa uandaaji wake kwa Manispaa ya kinondoni, Bi.Febronia Luyagaza, kwa niaba ya mchumi amesema, kabla ya mchakato wa bajeti kuanza yapo mfunzo yanayotolewa kwa lengo la kumsaidia Mkuu wa idara na Afisa bajeti kuibua vipaumbele atakavyovitekeleza ikiwa ni pamoja na kumsaidia muandaaji kuibua majukumu katika maeneo yake.
Aidha amewasisitiza wakuu wa idara na vitengo kuhakikisha wanashiriki mchakato wa uandaaji wa bajeti ili kuepukana na malalamiko yanayotokea kuhusiana na kuondolewa baadhi ya kazi au kupunguzwa kwa fedha kwenye kazi iliyobajetiwa.
Semina hii imepata uwakilishi kutoka WAMATA, Right to Play, SISEMA na waku wa Idara na vitengo.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari.
Manispaa ya kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.